Monday, 23 May 2011

BALOZI WA UGANDA NORWAY WAIPONGEZA ZANZIBAR

Balozi wa Uganda, Norway waipongeza Zanzibar

Na Abdalla Ali
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi jana lifanya mazungumzo na Mabalozi wawili wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.
Makamu huyo awali alikutana na Balozi wa Uganda nchin Tanzania, Ibrahim Mukiibi, na baadae kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Ingunn Klepsvik.
Katika mazungumo na Mabalozi hao, waliahidi kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi hizo na kuipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa kwa malengo yake ya kuweka maslahi ya watu wake mbele.
Kwa upande wake Balozi Mukiibi alisema uchaguzi wa nchini humo uliomalizika hivi karibuni ulikwenda vizuri na chama tawala kilishinda kwa zaidi ya asilimia 70 kwa ushindi wa jumla pamoja na Wabunge, ambao umewezesha kuwapa nguvu za utawala.
Aliziomba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuimarisha uhusiano wao wa kihistoria katika kuwaletea maendeleo watu wa nchi hizo.
Naye Balozi wa Norway, Klepsvik aliisifu Zanzibar kwa kuanzisha muundo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imesaidia kuleta utulivu nchini.
Kuhusu uundwaji wa serikali hiyo, Makamu wa Pili alisema hadi sasa ingawa ni muda mfupi lakini wanakwenda vizuri na wanaafikiana vyema katika malengo yao.
Alisema serikali ya imeundwa kwa mashirikiano na wameweka vipaumbele vya kilimo, afya na utalii ili kuimarisha uchumi na kuharakisha maendeleo ya ustawi wa wananchi.

No comments:

Post a Comment