Sunday, 8 May 2011

AJALI FEKI YAZUA TAFRANI

Ajali ‘fake’ yazua tafrani

Na Haroub Hussein
SEHEMU kubwa ya Manispaa ya Zanzibar ilikuwa kwenye taharuki kubwa baada ya kupatikana kwa taarifa za kutokea mripuko na kuwaka moto Bandari ya Zanzibar iliyopo eneo la Malindi mjini hapa.
Taarifa za kutokea kwa mripuko huo, zilisambaa majira ya saa nane na nusu mchana wakati magari ya kubebea wagonjwa, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi na Jeshi la Polisi kuonekana yakihamanika kufanya uokozi kwa kubeba majeruhi kuwapeleka katika hospitali ya Mnazimmoja.
Hata hivyo taarifa za uhakika ni kwamba ajali hiyo ilikuwa ni igizo ambalo liliandaliwa na Shirika la Bandari katika kuzipima taasisi na vikosi katika utoaji wa huduma za dharura pale janga kama hilo linapoweza kutokea.
Mwandishi wa Habari hii aliekuepo karibu na Bandari hiyo alishuhudia harakati hizo, na alipofika eneo husika alishughudia vijana wa Chama cha Msalaba mwekundu (Red Cross) wakiwabeba majeruhi na kuwakimbiza katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Aidha vikosi kama vile polisi, Zimamoto vikijivinjari na kuwa makini kama vile si ajali ya igizo, huku pia barabara zinazoelekea katika bandari hiyo zikifungwa.
Baada ya kumalizika kwa hilo lililodumu kwa takriban dakika 20, Mdhibiti wa Bandari ya Zanzibar, Sarboko Makarani Sarboko aliliambia Gazeti hili kuwa ajali hiyo ilikua na lengo la kujiangalia kwa Bandari pamoja na taasisi zote wanazoshirikiana nazo katika kazi zao za kila siku,akizitaja taasisi zinazofanya kazi ndani ya Bandari hiyo kuwa ni KMKM, Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa,TRA,ZRB na Afya.
Aidha alisema kwa Taasisi zilizo nje ya Bandari kuwa ni Red Cross, Zimamoto, Hospitali ya Mnazimmoja na Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo alipongeza kuwa zoezi hilo lilifanikiwa kwa kiasi kibwa mno ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Alisema katika mazoezi kama hayo kulikua na uvujishaji wa taarifa hivyo kukosa kujifanyia tathmini kwani taasisi nyingi zilikua zishajitayarisha tofauti na hili la mara hii.
Alisema kufanyika kwa zoezi hilo kunakwenda sambamba na masharti ya vigezo vya kimataifa vya Bandari na meli ambavyo vinasimamiwa na Marekani, na tayari Shirika la Bandari la Zanzibar lilikua limepewa siku tisini liwe limeshafanya zoezi hilo au litaondilewa katika Biashara za Kimataifa kwa kukosa vigezo hivyo vilivyowekwa ulimwenguni.
Sarboko alivizipongeza Taasisi zote zilizohusika katika kwa kuweza kufanikisha vizuri na kuvitaka kuendelea kufanya kazi kwa kukaa tayari na ajali mbali mbali zinazoweza kutokea katika Bandari za Zanzibar ili zinapotokea waweze kuokoa maisha ya watu na mali zao.

No comments:

Post a Comment