Friday, 6 May 2011

MANAHODHA WATAKIWA KUTOA TAARIFA.

Manahodha watakiwa kutoa taarifa za hitilafu

Na Rahma Suleiman, MCC
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya usafiri Baharini, Injinia Haji Vuai Ussi amewataka manahodha wa vyombo vya usafiri kutoa taarifa endapo wataona dalili zinazoweza kuleta athari kwa vyombo vyao wanapokuwa safarini.
Injinia Ussi alisema hatua ya kutoa ripoti pale vyombo vinapopata hitilafu baharini itasaidia uokozi na kunusuru maisha ya abiria na mali zao.
Mkurugenzi huyo alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Malindi mjini hapa.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa manahodha wa vyombo vya baharini kutoa taarifa pale inapotokea hitilafu kwenye vyombo vyao, jambo ambalo pia husaidia kupunguza hofu kwa wasafiri na jamaa zao.
Kauli ya Mkurugenzi huyo imekuja kufuatia meli ya M.V Serengeti wiki iliyopita kusafiri kwa muda wa saa 13 ikitokea Pemba hatua ambayo ilizusha hofu miongoni mwa wasafiri ndugu na jamaa.
Akizungumzia kadhia ya meli hiyo, Mkurugenzi huyo alisema kuchelewa kufika kwa meli hiyo kunatokana kuharibika kwa injini moja jambo ambalo lilisababisha mwendo wake kuwa mdogo na kuchelewa.
Injinia Ussi alisema hitilafu zilizojitokeza katika meli hiyo zinatokana na mabadiliko ya hali ya hewa na bahari kuchafuka kwa upepo wa dhoruba iliyotokea baharini.
Alisema meli ya M.V Serengeti kabla ya kuanza safari haikuwa na hitilafu yoyote kwenye injini zake, isipokuwa ilipata hilitafu wakati ikiwa safarini jambo ambalo lilikuwa gumu kuzuilika na linaloweza kutokea kwa vyombo vya usafiri.
Alifahamisha kuwa kila baada ya miezi mitatu Mamlaka hiyo kuzifanyia ukaguzi meli zote ili kuweza kubaini kama zina matatizo na pale zisipogunduliwa kuwa hitilafu huruhusiwa kufanya safari zake.
Hata hivyo alisema kuwa meli hiyo kwa sasa inafanyiwa matengenezo na itaruhusiwa kufanya safari baada ya kutengenea na kuhakikisha imekaguliwa kuwa ipo sahihi ndipo itakapoanza kufanya safari zake.

No comments:

Post a Comment