Friday, 6 May 2011

VIONGOZI MUWETAYARI KUFANYA KAZI PAMOJA -DK. SHEIN.

Viongozi muwetayari kufanyakazi pamoja-Dk. Shein

Awataka watendaji, wanasiasa kuwajibika
Akumbusha wajibu kuwaletea maendeleo wananchi
Rajab Mkasaba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ili kuwaletea wananchi maendeleo wanayoyatarajia ni lazima viongozi wawe tayari na wafanyakazi na kushirikiana pamoja.
Dk. Shein aliyasema hayo jana wakati akifungua semina ya siku tatu ya viongozi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na watendaji wakuu, inayofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Dk. Shein alisema madhumuni ya semina hiyo ni kuwajenga viongozi wanasiasa na watendaji wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa na mahusiano na mashirikiano ili hatimae kuwe na timu moja yenye ari ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo ya wananchi.
Alisema endapo viongozi hao watafanyakazi kama timu moja wataweza kuwatumikia vizuri wananchi na uchumi utakua kwa kasi huku pia utawala bora kuchukua nafasi yake.
Aidha alisema semina hiyo inatoa fursa viongozi kukutana na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya nchi ili hatimae wawe na mtazamo na mwelekeo mmoja katika kutumikia wananchi wote.
Alieleza kuwa wananchi wamejenga matumani makubwa kwamba serikali ya awamu ya saba, yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa, itawaletea maendeleo makubwa na ya haraka na wahusika wakubwa wa kufanikisha maendeleo hayo ni viongozi hao pamoja na wanasiasa.
Aidha Dk. Shein alifahamisha kuwa semina hiyo inatoa fursa kwa watendaji wakuu na viongozi wa kisiasa kuendeleza mkakati wa utekelezaji wa changamoto mbalimbali zilizopo katika Mawizara pamoja na kutafuta njia za kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.
Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao juu ya wajibu wa kutekeleza kila wawezalo ili kuhakikisha kuwa uchumi unaimarika zaidi na pia wanazingatia utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Sambamba na hayo, alisema anamatumaini kwamba pamoja na mambo mengine, semina hiyo ya siku tatu itawawezesha viongozi hao kuelewa wajibu wao na mipaka yao katika kutekeleza majukumu yao.
Pia, alieleza kuwa viongozi hao katika semina hiyo wataelewa misingi ya uhusiano na mbinu za kukuza uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa kisiasa na watendaji wakuu ambayo ni muhimu katika kutekeleza majukumu ya viongozi na watendaji.
Dk. Shein alitoa shukurani maalum kwa sekretariati ya Jumuiya ya Madola yenye Makamo Makuu yake jijini London, Uingereza na hasa Dunstan Maina kwa mashirikiano ya kufanikisha semina hiyo.
Kwa upande wake Dunstan Maina akitoa salamu kutoka Jumuiya ya Madola alisema kuwa Jumuiya hiyo itaendelea kuunga mkono nchi wanachama wake katika juhudi zake za kuimarisha uchumi na kupambana na umasikini.
Alisema kuwa juhudi kubwa zinahitajika katika kupambana na umasikini na kukuza uchumi kwa nchi za bara la Afrika.
Pamoja na hayo Maina alitoa pongezi kwa wananchi na viongozi wote wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendeleza amani na utulivu nchini.

No comments:

Post a Comment