Tuesday, 17 May 2011

OMANAIR YAAZA SAFARI MOJA KWA MOJA ZANZIBAR

‘Oman Air’ yaanza safari za moja kwa moja Zanzibar

Na Mwanajuma Abdi
SAFARI za anga kutoka Oman hadi Zanzibar zimeanza ramsi jana baada ya ndege ya shirika la Oman ‘Oman Air’ kutua katika uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wa Zanzibar.
Hayo yamebainika katika hafla ya uzinduzi wa ndege ya ‘Oman Air’, iliyofanyika katika hoteli ya Serena Inn iliyopo Shangani mjini hapa.
Ndege ya kwanza iliwasili Zanzibar jana asubuhi, ambapo iliteremsha abiria 65 na kupakia abiria 40, ikielekea na safari yake ya Oman kwa kupitia Dar es Salaam.
Sherehe maalum ilifanyika kiwanjani hapo kwa ngoma za asili na viongozi mbali mbali kuhudhuria akiwemo Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud.
Balozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar, Majid Alabadi alisema Oman imeamua kurejesha ndege hiyo kutokana na hali ya uwanja wa ndege wa Zanzibar kuimarishwa vizuri pamoja na kuwepo kwa usalama wa uhakika.
Alieleza uwanja wa Abeid Amani Karume umefanyiwa matengenezo makubwa na umeimarishwa kwenye utoaji wa huduma pamoja na suala zima la usalama.
Balozi Alabadi alifahamisha kuwa nchi ya Oman inajivunia mahusiano ya kidugu na kimawasiliano ya muda mrefu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Wazanzibari.
Alisema shirika hilo kurejesha huduma zake moja kwa moja hapa Zanzibar litasaidia kukuza biashara ya utalii.
Nae Katibu Mkuu wa Miundombinu na Mawasiliano, Dk. Vuai Lila alisema uwanja huo umeimarishwa kwa kufanyiwa matengenezo na kuzidishwa njia ya kurukia ndege, ili ndege kubwa na ndogo zituwe bila ya wasiwasi.
Aliongeza kusema kwamba, ujenzi wa ukuta (uzio), unaendelea ili kuweka usalama na ulinzi wakati wa ndege zinapotua na kuruka, sambamba na ujenzi wa jengo la abiria la kisasa, ambapo litakamilika baada ya mwaka mmoja na nusu.
Shirika la ‘Oman Air’ litafanya usafiri wa moja kwa moja kutoka Oman hadi Zanzibar mara tatu kwa kwa siku za Jumatatu, Jumanne na Jumamosi, ambapo ndege itakuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 156.

No comments:

Post a Comment