Sunday 8 May 2011

MADHARA YA KEMIKALI HARIBIFU YAELEZWA

Madhara ya kemikali haribifu yaelezwa

Na Riziki Abraham, Arusha
WADAU wa mazingira nchini wametakiwa kupunguza ama kutokuzalisha kemikali haribifu ambazo zina athari kubwa kwa mazingira na viumbe hai, ambapo kufanya hivyo watakuwa wametimiza hatua za kutekeleza mkataba wa Stockholm ulioridhiwa mwaka 2001.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Twariel Mchome, alisema hayo jana wakati akifungua warsha ya siku mbili jijini Arusha yenye lengo la kukuza ueledi kwa wadau mbalimbali wa mazingira nchini.
Alisema hivi sasa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kuweza kukabiliana na tatizo linalotokana na kemikali haribifu kwa mazingira.
Mchome alibainisha kuwa kemikali hizo zimekuwa zikizalishwa kwa kujua ama kutokujua na wananchi kutokana na shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo, ikiwemo uchomaji taka ovyo, hasa za hopitalini na viwandani kwa kutumia mitambo isiyo bora.
Nae, Mkurugenzi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Julius Ningu, aliwataka baadhi ya wafanyabiashara kuongeza uaminifu kwa kuingiza bidhaa zenye ubora unaotakiwa ili kukidhi viwango, hasa kwa kemikali zinazotumika katika shughuli za viwanda, kilimo na hospitali ikiwa ni pamoja na kutokuingiza madawa yaliyopitiliza muda wake.
“Ninasema ni vizuri wafanyabiasha wakaingiza nchini bidhaa zenye viwango vinavyotakiwa hasa kwa upande wa kemikali mbalimbali zinazotumika katika njia za uzalishaji ili kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira nchini”, alisema Dk. Ningu.
Aidha, alibainisha madhara mbalimbali ambayo hutokana na uzalishaji wa kemikali hizo unaweza kusababisha magonjwa kama saratani ya ngozi, mabadiliko katika mfumo wa kinga, madhara katika mfumo wa fahamu pamoja na madhara katika mazingira ambayo huathiri hata kiwango cha uzalishaji kutokana na udongo kupoteza ubora wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi, kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Magdalena Mtenga alisema ni vyema wananchi wakatambua kuwa hivi sasa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na baadhi ya kanuni zipo na zitaanza kuwabana wale wote wanaoingiza ama kutumia kemikali hizi hatarishi.
“Najua ni kweli baadhi ya kemikali hatarishi bado zinaingizwa nchini, lakini kwa kibali maalum mfano matumizi ya kemikali aina ya DDT ambayo bado yanaruhusiwa kuingizwa kutokana na matumizi yake katika nyanja ya utafiti pamoja na matumizi yake katika kuulia mazalia ya mbu nchini”,alisema.
Warsha hiyo ya siku mbili yenye lengo la kukuza weledi wa masuala ya kudhibiti kemikali haribifu kwa mazingira na viumbe imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, ikiwa imeshirikisha wadau mbalimbali kutoka Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment