Saturday 14 May 2011

ATAEPATA UONGOZI CCM KWA RUSHWA KUEGULIWA - BALOZI SEIF

Ataepata uongozi CCM kwa rushwa kuenguliwa – Balozi Seif

• Asema uvuaji gamba umeletwa na tuhuma za ufisadi
Na Abdulla Ali, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Seif Ali Iddi amesema nia ya Chama hicho ya kujisafisha ilitokana na tuhuma mbali mbali za wananchi juu ya ufisadi wa baadhi ya viongozi wake na kupelekea kupata ushindi mdogo katika uchaguzi uliopita.
Balozi Seif alieleza hayo alipozungumza na viongozi wa CCM kisiwani Pemba, akiwa katika ziara ya siku mbili ya kikazi.
Kwa hivyo alisema CCM imejivua gamba kwa kupanga safu mpya ya uongozi na watendaji wake pamoja na kuachana na njia zote zinazopelekea kushawishi rushwa wakati wa kutafuta viongozi.
Hivyo aliwataka viongozi kuwa makini katika chaguzi mbali mbali na kuwachaguwa viongozi kutokana na uwezo wao, sifa za utendaji na za kielimu ukiwemo uadilifu na kuwaepuka wanaotumia fedha au pochi kujipatia madaraka.
“Kamati ya maadili kamwe haitaridhia mtu yeyote kujipatia uongozi kwa rushwa na ata bainika watamuenguwa pasi na muhali,” alisema Balozi Iddi.
Wakati huo huo Balozi Seif amewataka wafanyakazi wa ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kufanya kazi kwa bidii kufanikisha kazi za Mtendaji Mkuu wa Serikali.
Hayo yalieleza katika mkutano wake na wafanyakazi wa Ofisi yake ya Pemba uliofanyika katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Pemba.
Alisema akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar anataka wafanyakazi wa Wizara yake wawe ni mfano wa utendaji bora.
Aliwataka wajitahidi kuimarisha umoja, upendo miongoni mwao na kuachana na majungu na fitina kwa lengo la kurahisisha utendaji wao.
Balozi Iddi alieleza kuridhishwa kwake na utendaji mzuri wa Ofisa Mdhamini wa Wizara hiyo, Amrani Massoud kwa usimamizi wake mzuri uliopelekea kuwa na ufanisi bora katika ofisi ya Pemba bila ya matatizo.
Aidha, aliahidi kuwapatia mafunzo kwa awamu wafanyakazi wa Ofisi hiyo na kurekebisha masuala mengine kadri bajeti itakavyoruhusu.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Meja mstaafu, Juma Kassim Tindwa aliupongeza utendaji wa Ofisi hiyo na kusema umekuwa wa mfano na kuzitaka ofisi nyengine kisiwani humo kuiga.
Kabla ya hapo Balozi Seif, alikutana na wafanyakazi wapya wa Wizara ya Afya waliopelekwa Pemba kuanza kazi, ambapo aliwapongeza kwa kuonesha uzalendo wao na kukubali kutimiza wajibu wao kufanya kazi popote nchini.
Alisema Zanzibar ni Pemba na Unguja, hivyo waajiriwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya kazi Pemba ni wajibu na sio adhabu kama inavyotafsiriwa na baadhi yao.
Nae Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya alionya juu ya wafanyakazi wataorejea Unguja bila ya ruhusa kuwa hawatopata fursa ya kuajiriwa tena.
Halikadhalika, alieleza umuhimu wa ajira kwao kwani alisema hata hiyo ajira yao imetokana na jitihada kubwa za Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Iddi ya kuomba wapatiwe fursa hiyo mbali ya kuwepo hali ngumu ya kifedha.

No comments:

Post a Comment