Friday, 6 May 2011

WAPINZANI MSIIGE UJASIRI WA KUVUA GAMBA.

‘Wapinzani msiige ujasiri wa kuvua gamba’

Na Mwandishi Wetu
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, amesema kitendo cha chama hicho kujivua gamba ni hatua ya kijasiri na wala kisitokee chama cha upinzani kuiga mfano huo.
Vuai alieleza hayo kwa nyakati tofauti huko kisiwani Pemba, alipokuwa akizungumza na wazee, watendaji na watumishi wa CCM na Jumuia zake kuangalia uhai wa chama kisiwani humo.
Alisema CCM, ilifikia hatua ya kujivua gamba na kujisafisha maamuzi ambayo ni magumu na ya kijasiri na wapinzani hawakutarajiwa kutokea.
Alifahamisha kuwa katika Afrika CCM ndiyo chama pekee kilichodumu kwa muda mrefu madarakani kwa kutumia uzoefu wa kisiasa, kura za kidemokrasia na mabadiliko yanayofanyika hivi karibuni yatakifanya chama hicho kuimarika zaidi.
Nao wazee na wafanyakazi wa CCM wa mikoa miwili ya Pemba walisema hatua ya kujivua gamba ni ya kupongezwa ni imedhamiria kukiimarisha nguvu za chama hicho na kuipongeza Halmashauri Kuu kwa uteuzi wa sekretarieti mpya.
Walisema safu hiyo mpya itaweza kusimamia vyema masuala ya kiuchumi na kisiasa na hatimaye kuleta maendeleo makubwa ndani ya chama hicho na taifa kwa ujumla.
Wakati huo huo, Naibu katibu huyo amewataka viongozi wa Jumuiya ya vijana ya chama hicho UVCCM kutumia vikao vya kikatiba kukosoana na kuelimishana kwa lengo la kukiimarisha chama hicho.
Aidha aliwataka watumie muda katika kutafuta elimu ili kukuza viwango vyao hali itakayowawezesha kwenda sambamba na karne ya 21 ya sayansi na teknolojia.

No comments:

Post a Comment