Tuesday 17 May 2011

MKUTANO WA KIMATAIFA UJASIRIAMALI KUKUZA MAENDELEO

Mkutano kimataifa ujasiriamali kukuza maendeleo

Na Mwanajuma Abdi
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mwanamwema Shein amesema mkutano wa kimataifa wa kujadili harakati na shughuli za wanawake utasaidia kukuza maendeleo ya akinamama na uchumi wa nchi.
Alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa siku moja wa kimataifa wanawake ulioandaliwa na Jumuiya ya ZAYEDESA, chini ya Mwenyekiti wake, Mama Shadya Karume ambao umewakutanisha wanawake wa Zanzibar, Jamhuri ya Czech na Jamhuri ya Slovak.
Mkutano huo wa siku moja wa wafanyabishara wadogo wadogo, wanawake, NGOs na utalii ulifanyika katika hoteli ya Waridi Beach Resort, Pwani Mchangani.
Alisema majadiliano yatakayofanyika katika mkutano huo yatasaidia kuleta maendeleo kwa wanawake kwa kupata taaluma, huku pia akitumia fursa hiyo kuelezea wanawake wa Zanzibar jinsi wanavyojiimarisha katika kuondokana na umasikini.
Mama Shein alisema maendeleo na hatua walizopiga wanawake wa Zanzibar yanatokana na kuimarika kwa amani na utulivu, huku akiwashajiisha wageni hao kutembelea sehemu mbali mbali za kihistoria ikiwemo Mji Mkongwe, ambako watajionea kazi zinazofanywa na akinamama.
Alizipongeza juhudi za ZAYEDESA kwa kuwezesha mkutano huo kufanyika Zanzibar, ambapo utasaidia kuwanyanyua kielimu wafabiashara wadogo na kuwaongezea ufanisi katika shughuli za kijasiriamali.
Nae Mwenyekiti wa ZAYEDESA, Mama Shadya Karume akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, alisema wanawake wajasiriamali wa Zanzibar wanakabiliwa na changamoto mbali mbali zinazokwamisha juhudi zao za kimaendeleo ikiwemo ukosefu wa elimu ya biashara, hali inayosababisha kutokuwa wabunifu.
Alisema changamoto nyengine ni suala zima la kutokuwa na soko la uhakika la kuuza bidhaa zao wanazozalisha, huku pia kukiwa tabia potofu kuwa suala la ujasiriamali ni la wanaume na si la wanawake.
Shadya alisema pia wajasiriamali wa Zanzibar wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la mitaji midogo pamoja na uwezo wa kutimia teknolojia za kisasa katika kuongeza ufanisi wa biashara zao.
Alieleza wanawake wengi wamejiajiri katika shughuli mbali mbali kwa ajili ya kujiletea maendeleo ya na nchi kwa ujumla licha kuzongwa na majukumu ya kuhudumia familia zao.
Shadya Karume alisema baadhi ya shughuli wanazojishughulisha ni pamoja na uuzaji wa bidhaa mbali mbali za kazi za mikono, ukulima, uuzaji wa vyakula na kufanya kazi za elimu na afya.
Hata hivyo aliwashukuru Jamhuri za Czech na Slovak kwa kukubali kuja kuungana na wananchi wa Zanzibar kwa kuikubalia Jumuiya ya ZAYEDESA kwa kuzidisha mashirikiano yao katika kuhudhuria mkutano huo.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Czech, Alena Gajduskova alisema wanawake wa huko wamepiga hatua kubwa kutokana kupatiwa taaluma za shughuli za kibiashara pamoja na kuwepo progamu maalum za wanawake katika kuwanyanyua kiuchumi.
Naye Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman alisema wanawake wa Zanzibar wamepata muamko katika shughuli za kujiletea maendeleo yao na kuondokana na umasikini.
Alisema juhudi za serikali ni kuwajenga kitaalum ili waweze kuifanya miradi yao na vikundi iwe endelevu.

No comments:

Post a Comment