Friday, 6 May 2011

UHABA WA VIFAA VYA UPASUAJI WAIKABILI CHAKECHAKE.

Uhaba wa vifaa vya upasuaji waikabili Chake-Chake

Na Zuwena Shaaban, Pemba
DAKTARI dhamana wa hospitali ya Chake-Chake, Sauda Kassim Omar, amesema kukosekana kwa baadhi ya vifaa vya operesheni katika hospitali hiyo kunasababisha kudorora upasuaji.
Dk. Sauda alisema kukosekana kwa vifaa hivyo kumekuwa kukisabisha kutofanyika upasuaji ambapo unaofanyika hivi sasa ni ule wa dharura tu.
Dk. Sauda aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na uongozi wa Pemba Press Club, pamoja na waandishi wa habari wakati walipofanya ziara hospitalini hapo kwa kuwafariji wagonjwa na kutoa zawadi kwa watoto waliyozaliwa siku ya uhuru wa vyombo vya habari.
Alisema gauze na bendeji ni vifaa muhimu katika kufanya upasuaji na kukosekana kwa vifaa hivyo kumezoretesha suala zima la upasuaji.
Alifafanua kuwa mbali na changamoto hiyo pia uchakavu wa vifaa nalo ni tatizo sugu ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka ili hospitali hiyo iweze kutoa huduma kwa wagonjwa wanaofikishwa wakiwa na matatizo mbalimbali.
Alifahamisha kuwa hivi sasa hospitali hiyo imekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa upasuaji hali inayotokana na kutokuwepo kwa madaktari wa upasuaji katika hospitali za Wete na Mkoani.
“Tatizo la uhaba wa nyenzo za upasuaji linachangiwa mno na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa upasuaji, ambapo mzigo mkubwa umeiangukia hospitali hii kutokana na hospitali za Mkoani na Wete kutokuwa na madaktari wa upasuaji”, alisema Dk. Sauda.
Dk. huyo aliueleza uongozi huo wa Pemba Press Club kuwa mbali na kutoa zawadi hiyo lakini pia wafikirie mbinu nyengine ya kuweza kufanya katika kusaidia suala zima la kupiga vita adui maradhi.
Kwa upande wake ofisa Mdhamini, wizara ya Ustawi wa Jamii maendeleo ya vijana, wanawake na watoto Pemba, Maua Makame Rajabu ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafala hiyo alisema jitihada zinahitajika katika kuondoa tatizo hilo kwani linaweza kusababisha kuambukizana magonjwa kwa akinamama hao pamoja na watoto wao.
Ofisa huyo aliwataka akinamama hao kuweza kuwatunza ipasavyo watoto wao na huku wakiwalea katika maadili mazuri na kutokuzipoteza haki za mtoto ambazo haki hizo ni nyenzo za kumlea na kumuweka katika maisha mazuri ya sasa na baadae.
“Sisi tunaiomba Wizara liiangalie hili kwani kulala kitanda kimoja wazazi wawili ni vigumu sana lakini kwa sasa hatuna la kufanya na tumelazimika kukaa hivyo kutokana na afya zetu, kwani hivi tunaweza kuambukizana magonjwa mbali mbali ya maambukizo ambayo yatakuwa hayana kizuwizi kwani kila mtu na afya yake Mungu aliyemjaalia nao”,walisema akinamama hao.
Jumla ya watoto wapatao 14 walizaliwa katika siku ya uhuru wa habari duniani katika hospital ya Chake-Chake.

No comments:

Post a Comment