Friday 20 May 2011

C-WEED YAIOMBA SERIKALI ILIPE UMUHIMU ZAO LA MWANI

C-weed yaiomba serikali ilipe umuhimu zao la mwani

Na Kauthar Abdalla
KAMPUNI ya ununuzi wa mwani ya C-weed Corporation imeiomba serikali kufahamu umuhimu wa zao hilo nchini pamoja gharama wanazozitumia wakati wa usafirishaji.
Akizungumza na mwandishi wa habari meneja wa mahusiano ya jamii wa kampuni hiyo Makame Salum Nassor alisema kampuni ili kuweza kusafirisha bidhaa hiyo haina budi kutumia gharama kubwa kiasi ambacho kinarejesha nyuma maendeleo ya kampuni hiyo .
Alisema meneja huyo kuwa kampuni imefikiria kuanzisha viwanda vingi vya kuusanifu mwani huo kwa kutengenezea vitu mbali mbali lakini hatua hiyo imekuwa ngumu kutokana na kutokuwa eneo la kutosha la kujenga kiwanda hicho pamoja na uhaba wa mali ghafi za kutengenezea vitu hivyo.
Alisema kwamba kiwango cha uzalishaji wa mwani huo kwa Unguja hakitoshelezi kuanzisha kiwanda inahitajika zaidi ya tani 10,000 kwa mwaka ili kuweza kumudu mahitaji hayo lakini kwa sasa ni tani elfu saba kwa mwaka ambazo wanazipata kutoka kwa wakulima wa zao hilo.
Hata hivyo meneja huyo alielezea juu ya malalamiko ya muda mrefu ya wakulima wa mwani kuwa bei ndogo wanayouzia lakini alisema kwa kuwa biashara ni huru basi kila mfanyabiashara anaangalia uwezo wa biashara yake ndipo aweze kutoa bei ya kununulia kwa wakulima hao.
Aidha alifahamisha kuwa bei ndogo inategemea na mnunuzi anaenunua kutoka katika kampuni hiyo ambapo zaidi ni kutoka katika nchi za nje ikiwemo Marekani, China na Ulaya.
Hivyo aliwaomba wananchi pamoja na wakulima kuondoa dhana ya kusema kwamba wanadhulumiwa katika biashara hiyo ila ni hali ngumu ya biashara wanayokumbana nayo kwa makampuni ya nje wanayoyauzia.
Pia meneja huyo ameitaka serikali kukaa vikao vya mara kwa mara na wamiliki wa makampuni yaliopo nchini ili kujadili mambo mbali mbali yanayohusu zao hili ikizingatiwa kuwa ni zao linaloingiza pato kubwa nchini kwa lengo la kuwaboresha wakulima wote na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment