Tuesday, 10 May 2011

ASKARI MBARONI KWA WIZI

Askari mbaroni kwa wizi
Na Halima Abdalla
JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia askari wawili wa Kikosi cha KVZ, baada ya kutokea wizi wa pisi 500 za televishemi na redio 50 na vitu vyengine katika ghala moja lililopo Kisauni lililokuwa likilindwa na askari hao.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Azizi Juma Mohammed, alisema ghala hilo lilivunjwa usiku wa Mei 7 mwaka huu katika eneo la Kisauni na kupelekea kuibiwa kwa vitu hivyo.
Aidha alisema walinzi wa ghala hilo walikuwa askari wawili wa KVZ ambao majina yao yamehifadhiwa na mmiliki wa ghala hilo ni Ramadhan Simai Makame Mkaazi wa Mwanakwerekwe Mjini Zanzibar.
Alisema Jeshi la Polisi linatafuta gari lililohusika kupakia mizigo iliyoibiwa kwenye ghala hilo, huku likisaka watuhumiwa wengine waliohusika.
Wakati huo huo watu wawili wamefariki dunia baada ya kukamata paipu ya antena ambayo iliyokuwa na shoti ya umeme.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Azizi Juma Muhammed aliwataja watu hao waliofariki kuwa ni Asha Yussuf Shehe (20) na Muhammed Abdalla Awadh (23) ambao wote ni wakaazi wa Muembeladu.
Alisema mmoja wa marehemu kabla hajafa alikuwa akizungusha antena baada ya kuona TV yake haioneshi vizuri baada ya kuzungusha alinasa na kupelekea kufa ndipo akatokea mwenziwe kwa ajili ya kutaka kumnasua na yeye kunaswa na umeme huo na kufa.
Kamanda alisema kuwa watu hao baada ya kufariki dunia walifikishwa katika hospitali ya Mnazi mmoja kwa ajili ya kuangaliwa ambapo daktari aliweza kuthibitisha vifo vyao.

No comments:

Post a Comment