Monday, 9 May 2011

MABANDA 73 YA BIASHARA YACHOMWA MOTO KASKAZINI UNGUJA

Mabanda 73 ya biashara yachomwa moto Kaskazini Unguja

• Serikali yaagiza kuchukuliwa hatua wahusika
Na Abdulla Abdulla, OMPR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeviagiza vyombo vya usalama Zanzibar kulishughulikia ipasavyo suala la kuchomwa moto vibanda vya biashara katika fukwe za Pwani Mchangani na Kiwengwa.
Agizo hilo lilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alipofika katika maeneo hayo kuangalia hasara iliyopatikana na kuwapa pole waliopatwa na mkasa huo wa kuchomewa maduka yao.
Balozi Seif kwa niaba yake na Serikali kwa ujumla alieleza kusikitishwa kwake kuhusu vitendo hivyo na kuahidi kuchukua hatua zinazofaa kuvikomesha.
Aliwataka wamiliki wa maduka hayo kutolihusisha suala hilo na ubaguzi baina ya Watanzania Bara na Visiwani kwa dhana ya kuwa wengi wao wana asili ya Bara. Bali wajione kuwa ni Watanzania na wana haki ya kufanya biashara kama wenzao wanavyofanya kwao kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Kwa hivyo aliwapa pole kwa hasara waliyoipata na kuhusu pahali pa kujistiri kwa wakati huu, Balozi Iddi alisema Serikali ya Mkoa itawapatia sehemu ya kulala kwa muda.
Kabla ya hapo katika risala yao waathirika hao waliiomba Serikali kuchukuwa hatua zinazofaa dhidi ya wanaohusika badala ya kuwaona mitaani wakitamba na pia kuomba wapatiwe mahali maalum pa kujenga maduka yao ili waishi kwa amani.
Halikadhalika, katika shukrani zao zilizowasilishwa na mmoja wao, James Charles, zilimpongeza Makamu huyo wa Pili wa Rais na Serikali kwa ujumla kwa kufika kuwafariji na hatua wanazochukuwa juu ya kadhia hiyo.
Kiasi cha watu 40 wamechomewa maduka yao juzi ambapo mabanda 43 yalichomwa katika ufukwe wa Pwani Mchangani karibu na Hoteli ya Waikiki na 30 yalichomwa Kiwengwa karibu na Hoteli ya Ocean Beach Resort.

No comments:

Post a Comment