Saturday, 14 May 2011

ARSENAL ZENJ WAMFUTA MACHOZI WENGER

Arsenal Zenj wamfuta machozi Wenger

Na Salum Vuai, Maelezo
TIMU ya mashabiki wa Arsenal waliopo Zanzibar, wamefanikiwa kumfuta machozi Mzee Arsen Wenger aliyeshindwa kupata angalau kikombe cha ‘babu’ msimu huu, baada ya kuibuka bingwa wa ‘Serengeti Soccer Bonanza’.
Katika bonanza hilo lililofanyika jana kwenye uwanja wa Mao Dzedong likishirikisha vikosi vya wapenzi wa klabu nane mashuhuri za Ulaya, washika bunduki hao waliifumua Barcelona kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali.
Bao hilo la ushindi lilipachikwa kimiani na Mwita Iddi Shaaban kwa shuti la adhabu lililokwenda moja kwa moja nyavuni mnamo dakika za mwisho za mchezo huo.
Kabla kutinga hatua hiyo, Barcelona iliitoa nje Chelsea kwa magoli 2-0 huku Arsenal ikiifurusha Manchester United kwa changamoto ya mikwaju ya penelti baada ya wamaume hao kumaliza dakika 14 za mchezo bila kufungana.
Kufuatia ushindi huo, Arsenal ilizawadiwa kikombe pamoja na kitita cha shilingi laki tano, ambapo Barcelona walitia mfukoni shilingi laki tatu na kikombe kidogo.
Jumla ya timu nane za Ulaya ziliwakilishwa na mashabiki wao katika patashika hiyo iliyoandaliwa na vituo vya redio vya Coconut FM cha Zanzibar na kile cha Clouds FM chenye maskani yake jijini Dar es Salaam, na kudhaminiwa na kampuni ya Serengeti pia ya Dar.
Mbali na Arsenal na Barcelona, timu nyengine kwenye kinyang’anyiro hicho zilikuwa Manchester United, Liverpool, Chelsea, Inter Milan, AC Milan pamoja na Real Madrid.
Bonanza hilo lililotanguliwa na maandamano ya timu zote yaliyoanzia viwanja vya Muembe Kisonge na kuongozwa na beni la mbwakachoka, yalivutia wapenzi wengi waliofurahia vipaji vya wachezaji wa hapa ambapo kila timu ilikuwa ikicheza na wachezaji saba kwa kutumia magoli yanayotumika kwa mpira wa mikono.

No comments:

Post a Comment