Sunday 8 May 2011

RAZA AZUNGUMZA KUJIVUA GAMBA, KATIBA MPYA.

Raza azungumzia kujivua gamba, katiba mpya

Na Salum Vuai, Maelezo
MFANYABIASHARA mashuhuri hapa Zanzibar, Mohammed Raza Dharamsi, amesema daima anaamini katika ukweli na hakuna mtu anayemtuma juu ya maoni anayotoa kuhusiana na mambo mbalimbali nchini yanayotokea nchini.
Raza alikuwa akizungumza na kituo cha televisheni ya taifa TBC One katika kipindi chake cha ‘Jambo Tanzania’ kilichorushwa jana asbuhi.
Alisema tatizo analoliona ni kwamba watu wengine hawapendi kuambiwa ukweli na wamekuwa wagumu kubadilika hata katika mambo yanayohusu maslahi ya umma.
Alieleza kuwa, kusema ukweli ndio silaha nzuri inayoweza kuondosha mafundo yaliyo ndani ya nyoyo za watu wanaoona zipo kasoro zinazohitaji kurekebishwa, lakini wenye mamlaka wanazipuuza kwa sababu ya kuangalia zaidi utashi wa nafsi zao.
Akizungumzia mabadiliko ya kisiasa yaliyozaa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, Raza alisema hiyo ni neema iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu kuwapelekea wananchi wa visiwa hivi, kwa kuwa imekuja kuwahakikishia amani na utulivu.
Alifahamisha kuwa mchakato wa kupatikana serikali hiyo ulianzia mbali mwaka 2008 katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mjini Butiama, ingawa kuwasili kwake kumekuja hivi karibuni.
Alisema kwa mwanahalali yeyote Mzanzibari na mwenye akili timamu, bila shaka hataacha kufurahia mabadiliko yaliyopo sasa ambayo yanatoa fursa kwa wananchi kufanya kazi za kujiletea maendeleo badala ya kukaa vijiweni kuoneshana vidole kuhusu tafauti za kisiasa.
Raza ambaye alijitokeza miongoni mwa wanachama wa CCM waliotaka kugombea uraisi wa Zanzibar mwaka jana, akitoa maoni yake kuhusu maamuzi ya kujivua gamba katika safu ya uongozi wa chama chake, alikisifu kitendo hicho na kusema ni cha ujasiri kwani chama kilikuwa kinaulekea kubaya.
“Mnapofika pahala mkipita njiani watu wanaoneshana vidole ‘ndiye yule mnamuona’, lazima mfanye busara ya kujitathmini na kutafuta sababu za hayo, kwa hili nampongeza Mwenyekiri wa CCM Kikwete kwa kusoma alama za nyakati
Alisema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa imezaa CCM mpya yenye kujali maslahi ya umma, kwani baadhi ya viongozi walikuwa wanapotoka kwa kuangalia zaidi tafauti za makundi, rangi na makabila katika kujenga nchi mambo aliyosema hayana nafasi katika ujenzi wa nchi inayojali utawala bora.
Akizungumzia serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Raza amesema mabadiliko yanayotokea nchini ni dalili ya ukomavu wa kisiasa uliopo hapa.
Alitoa mfano wa uchaguzi wa mwaka 2005 katika mfumo wa vyama vingi, ambapo huko Pemba wapiga kura walihiyari kuchagua ‘maruhani’ badala ya mtu halisi aliyekuwa na roho yake.
Hata hivyo, alidai kuwa matatizo mengi yanayotokea katika siasa za nchi hii, hutokana na ubinafsi wa baadhi ya viongozi wanaodiriki kuwatenga viongozi wastaafu ambao alisema wamefanya mengi katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Kuhusu mchakato wa maoni ya wananchi katika suala la marekebisho ya katiba, Raza hamasa kali zilizooneshwa na Wazanzibari zinatokana na udhaifu wa baadhi ya watendaji wanaomzunguka Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, kudharau nafasi ya upande mmoja na kufanya mambo kama wao ndio kaka mkubwa bila kuwashauri wahusika wakuu wa Zanzibar.
“Viongozi wakuu wa nchi hawana mataizo na ninaamini wana nia njema na muungano, lakini wanaangushwa na wapambe wanaowazunguka wasiotaka kutenda haki sawa kwa nchi zote mbili za Zanzibar na Tannganyika”, alifafanua.
Alieleza kuwa si jambo jema kumaliza mambo yote Karimjee na Dodoma bila kuwashirikisha Wazanzibari na baadae kuwaletea ujumbe dakika za mwisho, na kusisitiza kuwa muungano wa nchi mbili isiangaliwe kwa tafauti ya idadi ya watu na kuiona nchi moja kuwa ndio kubwa kuliko nyengine.
Alitoa wito kwa Watanzania na hasa viongozi kuhakikisha muungano unakuwa na maslahi kwa wananchi wa pande zote kama walivyokusudia waasisi wake hayati Julius Kambarage Nyerere na marehemu Abeid Amani Karume.

No comments:

Post a Comment