Tuesday, 10 May 2011

WASHUKIWA UTIAJI MOTO PWANIMCHANGANI WASHIKILIWA

Washukiwa utiaji moto Pwanimchangani washikiliwa
Na Mwantanga Ame
POLISI Mkoa wa Kaskazini Unguja imeanza kutia nguvuni wananchi wa kijiji cha Pwani Mchangani, huku ikipita   nyumba kwa nyumba kuwanasa  wanaoshukiwa kutia moto mabanda ya wafanyabiashara wa eneo hilo.
Hatua hiyo ya Polisi imekuja baada ya baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wapatao 40 hadi 50 kuunda kundi na kuamua kuyatia moto mabanda ya wafanyabiashara kwa madai yamekuwa yakitumika kinyume na maadili.
Wananchi hao wanadai kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakitumia sehemu hizo kwa kuuza vinywaji vya pombe, dawa kulevya na majani makavu yanayosadikiwa kuwa ni bangi.
Akizungumza na Zanzibar Leo Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Mselem Masoud Mtulia, alisema Polisi inaendelea na msako wa nyumba kwa nyumba kuwakamata washukiwa wa utiaji moto mabanda hayo, watu saba wanashikiliwa na jeshi hilo.

Waliokamatwa hadi jana ni Salum Faki Ame (60), Haji Ame Iddi (46), Mohammed Masoud Afadhali (21), Mohammed Haji Sheha (21), Machano Kijoka Ali (45) Mwinyi Abdalla Msanifu na Hassan Makame Chande (31).

Alisema watu hao wanadaiwa kutenda kosa hilo siku ya Ijumaa majira ya saa 10:30 jioni hadi saa 11.00 ambapo walifika katika maduka ya wafanyabiashara hao na kuazisha vurugu hizo ambapo Polisi baadae ilifika katika eneo la tukio na kukuta tayari watu hao wamekimbia.
Alisema Polisi itachukua hatua hiyo kutokana na uhalifu uliofanywa ni mkubwa kwa vile watu hao walichoma mabanda ya wafanyabiashara hao yakiwa na mali zao huku wengine wakiwa ndio sehemu ya nyumba walizokuwa wanaishi.
Aidha, Kamanda huyo  alisema uharibifu mwengine uliotokea ni pamoja na kutia moto mali za baadhi ya makampuni ya simu ikiwemo ya Tigo ambapo mnara wake umetiwa moto.
Kuhusu uthibitisho kama kweli wafanyabiashara hao wamekuwa wakifanya biashara zinazokiuka maadili alisema hilo hawana uhakika nalo kwani hakuna kesi wala malalamiko ya wanakijiji hao iliyowasilishwa katika vituo vya Mkoa wake kulalamikia hilo.
Alisema sehemu kubwa ya wafanyabiashara hao walikuwa wakijihusisha na biashara ya kuuza bidhaa za mahitaji ya nyumbani, vyakula vya Mama ntilie, vinyago, na picha za sanaa ya uchoraji maarufu kwa jina la tinga tinga.
Hata hivyo alisema kumekuwa na taarifa za wafanyabishara hao kutishiwa maisha kutokana na kupigiwa simu za vitisho pindipo wakiwataja kuhusika na tukio hilo.
Alisema wanaofanya vitendo hivyo Polisi, itawachukulia hatua kwani  ni miongoni mwa mambo yanayotishia amani ya nchi ambapo tayari serikali kuu kupitia Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi ambae alifika kwa ajili ya kuwapa pole na ameagiza kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa wale wote waliohusika na uvunjifu wa amani huo.
Kutokana na amri hiyo ya serikali Kamanda Mtulia alisema tayari baadhi ya wananchi hao wameamua kuingia mafichoni huku wengine kukimbia lakini Polisi itahakikisha inapita nyumba hadi nyumba na kuwakamata wahusika hao.
“Tunachotaka waeleze ukweli kwani hao watu wanajulikana na wametambuliwa na wafanyabishara wenyewe waliotiliwa moto sasa wasijidanga nyeye kama watawaficha tutapita nyumba hadi nyumba”, alisema Kamanda huyo.
Matukio ya utiaji moto maeneo ya biashara katika Mkoa wa Kaskazini yamekuwa yakitokea mara kwa mara baada ya baadhi ya wananchi kutoridhia na baadhi ya wafanyabishara kwa kisingizio wamekuwa wakipotosha maadili kutokana na kuuza pombe.
Ni miezi michache tu baadhi ya wafanyabiashara wa maeneo ya Kaskazini ‘B’ kijiji cha Kiwengwa walikutwa na kadhia ya kutiliwa moto maduka yao ambapo Makamu wa Pili wa Rais aliwafariji kwa kuwapatia fedha waadhirika wa tukio hilo.

No comments:

Post a Comment