Sunday 8 May 2011

WALIMU WAKUU WAJIWEKA KANDO MATOKEO MABOVU.

Walimu wakuu wajiweka kando matokeo mabovu

Ni ya kidato cha sita, nne, wawarushia mpira walimu
Na Mwanajuma Abdi
WALIMU wakuu wa skuli mbalimbali wamesema sababu za wanafunzi kuboronga katika mitihani ya kidato cha nne na sita, zinatokana na walimu kutokuwa tayari kufanyakazi wakililia maslahi duni.
Hayo yalielezwa katika kikao cha pili cha Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari (JUWASEZA), kilichofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Kazi za Amali huko Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Unguja.
Walisema walimu wa chini wanapowaona walimu wakuu hawapo katika mazingira ya skuli wanatumia nafasi hiyo kuranda na kufanya kazi zao binafsi badala ya kuwasomesha wanafunzi wakisingizia hali ngumu ya maisha.
“Sababu ya kufanya vibaya wanafunzi wetu wa Zanzibar, walimu hawajajidhatiti ‘committed’ kusomesha na badala yake wanatumia nafasi hiyo kufanya shughuli zao ikiwemo kwenda kusomesha masomo ya ziada kwa ajili ya kujipatia fedha”, walisema wachangiaji wa kikao hicho.
Walisema kasoro nyengine ni pamoja na wanafunzi kuwa wengi katika darasa moja ambapo hufikia hadi 80 hususani skuli za serikali kiasi ambacho walimu wanapata wakati mgumu wa kusomesha ukilinganisha na skuli za binafsi.
Hata hivyo walishauri Wizara ya Elimu kuweka skuli za kidato cha sita pekee kwani kuchanganya na madarasa mengine kunachangia walimu kukosa muda wa kumaliza silebasi za masomo katika kila mihula ya kidato cha pili, nne na sita, hali inayosababisha wanafunzi kufeli.
Akiwasilisha mada matokeo ya mitihani wa taifa, Katibu wa Jumuiya ya JUWASEZA, Khatib Tabia alisema matokeo ya taifa ya kidato cha pili, nne na cha sita Zanzibar kwa mwaka 2010 hadi 2011 ni mabaya, ya kuvunja moyo na kuyaita ya msiba.
Alifafanua kuwa, kidato cha sita miongoni mwa skuli 10 za mwisho zilizofanya vibaya kati ya idadi hiyo tano zimepatikana Zanzibar, hali ambayo inahitaji kufanyiwa tathmini ya hali ya juu ili kurejesha imani kwa wazazi kwa kuwasomesha watoto wao na kuweza kufaulu vizuri.
“Matokea ya kidato cha sita mabaya hivyo wanafunzi wataoingia vyuo vikuu vilivyokuwepo nchini watapatikana wapi?”, alihoji walimu wenziwe.
Katibu huyo, alizitaja baadhi ya kasoro zilizoweza kuchangia kufeli wanafunzi ni pamoja na udanganyifu ambao mara nyingi wanafanyika katika mitihani ya kidato cha nne kwa kukopia, jambo ambalo linasababisha kuzalisha wanafunzi bomu wanaoingia kidato cha sita.
Alifahamisha kuwa, sababu nyengine ni upungufu walimu wenye sifa za kufundisha kidato cha sita nako kunachangia kutofanya vizuri vijana pamoja na mfumo wa utoaji wa elimu nchini, hivyo alipendekeza kamati iliyopangiwa kazi hiyo iyazingatie kwa uangalifu masuala hayo ili yapatiwe ufumbuzi kwa kina.

No comments:

Post a Comment