Monday, 9 May 2011

KMKM YAMKINGIA KIFUA BUSHIRI

KMKM yamkingia kifua Bushiri

Na Donisya Thomas
NAHODHA wa timu ya soka ya KMKM, Ame Msimu, amesema, kocha Ali Bushiri, asibebeshwe lawama kwa timu yao kufanya vibaya katika michezo ya ligi ndogo ya Zanzibar.
Alisema, Bushiri, ni kocha mzuri na kamwe asihusishwe na KMKM kupoteza michezo kadhaa ya ligi kwani hiyo inatokana na ushindani mkubwa uliopo katika ligi hiyo.
Nahodha huyo wa KMKM aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na gazeti hili na kumkingia kifua kocha wake baada ya mashabiki wa klabu hiyo kusema ameshindwa kuipatia mafanikio timu hiyo katika michezo iliyokwishachezwa na hivyo kuambulia kichapo kila iliposhuka dimbani.
Aidha, alifahamisha, kuwa hakuna kocha yoyote duniani ambae anapenda kuona timu yake ikifungwa na kama yuko huyo basi atakuwa na matatizo ya akili na hivyo kusema kwamba Bushiri, asihusishwe kwa hilo la KMKM kufanya vibaya katika michezo yake ya Unguja.
" Hao wanaosema Bushiri hana jipya KMKM hawajui wanachokisema, kwani mchezo wa mpira wa miguu ni kama mchezo wa bahati nasibu leo unapata kesho unakosa" alisema mchezaji huyo mkongwe wa KMKM.
Hata hivyo, alikiri kwamba ligi ndogo ni ngumu kutokana kuchezwa katika mkondo mmoja kulinganisha na ligi kubwa kwani katika ligi ndogo ukipoteza mechi ndio imetoka tofauti na ligi kubwa ukipoteza mchezo katika mzunguko wa kwanza unaweza kujirekebisha mzunguko wa pili.
KMKM ambao waliwahi kutwaa ubingwa Zanzibar , inatarajiwa kuondoka hapa kwenda Pemba kucheza na timu za huko na itashuka dimbani Mei 10 dhidi ya Madungu.
Akizungumzia mechi za Pemba, mchezaji huyo alisema wanauhakika wa kufanya vizuri na kujiweka katika nafasi za juu ili waendelee kuwepo katika ligi kuu mwakani.
" Wachezaji wapo vizuri na wameahidi kufanya vema katika michezo yote ya Pemba" alifahamisha Msimu.
“ Mpaka sasa wachezaji wote wapo sawa ila tuna majeruhi mmoja, Gideon Brown ambae atabaki na kwa upande mwengine Ame Khamis 'Kibobea' nae alikuwa mgonjwa, lakini hadi jana alikuwa anaendelea vizuri hivyo tunaweza kuambatana nae kwenda Pemba kusaka pointi katika michezo yote”. alibainisha.
Aidha, alieleza, ligi ndogo imekosa mvuto huku mashabiki wachache kujitokeza viwanjani na hiyo imechangiwa na ligi kukosa udhamini.
Hivyo alitoa rai kwa ZFA kujipanga kusaka wadhamini wa kuendesha ligi ili kupunguza ukata kwa klabu sambamba na kuifanya ligi kuwa ya mvuto na ushindani zaidi.

No comments:

Post a Comment