Tuesday, 17 May 2011

DK. SHEIN:SERIKALI IMEANZA KUTEKELEZA AHADI ZAKE

Dk.Shein: Serikali imeanza kutekeleza ahadi zake

• Afungua kituo cha afya daraja la pili
Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali imeanza kutekeleza ahadi ya kuleta mabadiliko katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vya vya daraja la pili, hatua itayoipunguzia mzigo hospitali ya Mnazimmoja.
Dk. Shein, alisema hayo jana baada ya kukifungua rasmi kituo cha Afya daraja la pili cha Mpendae, ambacho kimejengwa kwa nguvu za wananchi, michango ya wahisani na viongozi wa Jimbo hilo.
Dk. Shein, alisema kufunguliwa kwa kituo ni ahadi ya serikali iliyoitoa wakati wa kampeni za kuleta mabadiliko katika sekta ya afya pamoja na kuipunguzia mzigo hosptali ya Mnazimmoja kwani iko katika hatua za kuwa ni hospitali ya Rufaa.
Alisema serikali itahakikisha inazitekeleza ahadi zake zote ilizozitoa na kuhakikisha mikoa yote Unguja na Pemba inakuwa na hospitali za daraja la pili ambapo tayari kwa mjini hospitali hizo katika Jimbo la Kwamtipura na Mpendae.
"Mtakumbuka katika kiwanja cha Garagara nilisema nitaviendeleza vituo vya afya vya Mpendae na Kwamtipura ambapo tutavijenga kwa kuvifanya kuwa ni vya daraja la pili, lengo ni kupunguza msongamano katika hospitali kuu ya Mnazimmoja”, alisema Dk. Shein.
Dk. Shein, aliwataka viongozi wa wizara pamoja na Jimbo hilo kuona wanatafuta njia zaidi zitazowawezesha kufanikisha ujenzi wa hospitali hiyo kwa awamu ya pili, huku pia akitoa wito kwa watendaji wa sekta hiyo kubadilika.
Mapema baadhi ya viongozi wa Jimbo hilo wakitoa maoni yao katika risala, walisema wanakusudia kuendeleza ujenzi huo kwa awamu ya pili baada ya ile ya kwanza kukamilika ambapo tayari huduma zimeanza kupatikana kituoni hapo.
Alisema ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kuwa wa ghorofa mbili ambapo utagharimu shilingi milioni 400, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi 152 zimetumika.
Wananchi hao waliiomba serikali kuwafikiria kuwapatia ajira walinzi wanaolinda kituo hicho na kuwaimarishia mfumo wa maji safi na pia kuishinikiza wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kumalizia ujenzi wa Skuli ya Sekondari katika Jimbo hilo.
Katika hatua nyengine Dk. Shein alitembelea kituo cha mtambo wa kuzalishia mbegu bora za madume ya Ng’ombe huko Maruhubi, na kuutaka uongozi wa wizara ya Mifugo na Uvuvi walidhibiti eneo la kituo hicho ili kuepuka uvamizi.
Dk. Shein, alisema nia ya serikali hivi sasa ni kuona sekta ya ufugaji inaimarika baada ya kuonekana huduma nyingi kufifia na kwamba serikali itaimarisha sekta hiyo.
Alisema maendeleo ya ufugaji ni moja ya mambo ya msingi ambayo serikali imedhamiria kuyakuza na kuwapo kwa mtambo unaotumika kuzalishia mbegu za ufugaji ni hatua itayokuza maendeleo kwa sekta hiyo.
Naye Mkuu wa kitengo hicho, Dk. Khamis Ibrahim, akitoa maelezo juu ya mtambo huo alisema tayari hivi sasa imeweza kuwapandishia ng’ombe 1,776 ambapo kwa upande wa Pemba ni 1,046 na Unguja ni 721 kwa mwaka.
Aidha, mtaalamu mwengine wa wizara hiyo Hafidh Said, alisema nia ya wizara hiyo kuona hivi sasa wanapunguza uagizaji wa ng’ombe wa kupandishia kutoka Arusha, kutokana na hivi sasa kuwepo kwa ng’ombe wawili wanaofanya kazi ya kutoa mbegu.
Akifanya uzinduzi wa kituo cha skuli cha Meya Dk. Shein, aliwataka wananchi kuona wanaendeleza kutoa michango yao katika kukuza sekta hiyo ya elimu kwani nia ya serikali kuona maendeleo ya elimu yanakuwa.
Alisema serikali ya awamu ya saba italiendeleza hilo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo uamuzi wa Rais wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, aliyeahidi kutoa elimu bila ya malipo kwa Wazanzibari wote.
Dk. Shein kwa kufanikisha maendeleo ya mradi huo ameahidi kutoa shilingi milioni 7,000,000 ikiwa ni mchango wake kwa ajili ya ujenzi huo ambapo hapo awali mratibu wa skuli hiyo Sichana Talib alisema bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali za kukamilisha mradi huo ikiwemo ujenzi wa kiwanja ambapo hadi sasa tayari wameshatumia milioni 30.
Mapema Dk. Shein alipokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za Mkoa wa Mjini Magharib ambapo ilieleza kuwa serikali ya mkoa imeweza kufanikisha miradi mbali mbali ya maendeleo huku kukiwa na changamoto mbali mbali za kuimarisha Mkoa ambapo aliwataka viongozi wa Mkoa kuendeleza jitihada hizo.
Aidha, Dk. Shein, alifanya ukaguzi katika kiwanja cha Mnazimmoja na kuutaka uongozi wa Baraza la Manispaa, kuliangalia suala la michirizi katika kiwanja hicho ikiwa ni hatua ya kukabiliana na tatizo la kujaa maji kwa wakati wote.
Kaimu Mkurugenzi wa Baraza hilo Mzee Khamis, alisema maji yanayokaa katika eneo hilo hivi sasa tayari baraza lake inalifikiria kulifanyia kazi baada ya kuonekana athari zake kuongezeka ikiwa ni hatua watayoifikiria kwenda sambamba na mradi wa mitaro wa maeneo ya Ng’ambu ambao utaanza karibuni.
Dk. Shein, ataendelea tena leo kufanya ziara yake hiyo, kwa kutembelea wilaya ya Magharibi, kwenye kituo cha utafiti wa kilimo Kizimbani, Ufunguzi wa nyumba ya daktari Kizimbani, Uwekaji wa Jiwe la Msingi la kituo cha Afya Mtoni na kukagua Kilimo cha Mpunga wa Kumwagilia maji.
Sehemu nyengine ambazo atarajiwa kuzitembelea ni ya Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya magharibi, Ufunguzi wa nyumba ya daktari Kombeni, kukagua uwanja wa timu ya Bweleo na uwekaji wa jiwe la msingi Skuli ya Maandalizi ya Bweleo.
Mikutano ya hadhara ambayo ilipangwa kufanyika katika ziara hizo Idara ya Habari Maelezo, imeeleza kuwa imefutwa.

No comments:

Post a Comment