Mbunge lawamani kukimbia mwaliko wa wasanii
Na Aboud Mahmoud
IMEELEZWA kuwa, sanaa ya filamu nchini Zanzibar, inashindwa kuendelea kwa kuwa viongozi wengi wa majimbo hawaoni umuhimu wa kuwasaidia wasanii hao wa filamu na maigizo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Sanaa ya Maigizo Zanzibar Haidhuru Filbert Haidhuru, amesema hayo wakati wa sherehe za uzinduzi wa filamu ya 'Nyakunguju' ziliyofanyika wiki iliyopita katika ukumbi wa skuli ya Haile Selassie.
Haidhuru alitoa mfano wa sherehe hizo ambapo aliyetarajiwa kuwa mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa jimbo moja lililoko Wilaya ya Mjini (jina tunalo), aliwaweka watu kwa muda mrefu wakisubiri ujio wake lakini akashindwa kutokea.
Hata hivyo, kwa kuwa alikuwa amealikwa rasmi kwa mwaliko wa mapema, uongozi wa jumuiya hiyo uliamua kumzindua kwa kumpigia simu majira ya saa 2:15 usiku, lakini kwa mshangao wa wengi, alijibu asingeweza kufika kwa vile alikuwa jijini Dar es Salaam.
"Kwa kweli sanaa ya maigizo visiwani kwetu haiwezi kwenda mbele kwani viongozi wetu majimboni wanaturudisha nyuma, wanatujua wakati wanapotaka kura tu lakini baada ya hapo hawana tena usuhuba nasi", alisema Mwenyekiti huyo.
Haidhuru alieleza kuwa, mbali na Mbunge huyo ambaye ni mfanyabiashara maarufu hapa nchini, pia waliwaalika viongozi mbalimbali wakiwemo Mbunge na Mwakilishi wa jimbo lao na lile jirani la Jang'ombe, lakini wote hawakufika.
Hata hivyo, sherehe za uzinduzi huo zilizojaza ukumbi, ziliokolewa na mwanahabari mwandamizi wa kituo cha ITV Maulid Hamad Maulid, aliyejikuta akivalishwa joho la kuwa mgeni rasmi mbadala.
Akizungumza katika hafla hiyo, Maulid alisema Zanzibar imejaaliwa kuwa na hazina kubwa ya wasanii wa fani mbalimbali, lakini wanashindwa kupiga hatua kutokana na kutopewa umuhimu na mamlaka zinazohusika ikiwa ni pamoja na viongozi wa majimbo kuwakimbia wasanii.
Aliwataka wasanii hao kutumia fursa ya kushiriki katika matamasha na kuingia mikataba na mahoteli ili kujitangaza, hali aliyosema itasaidia kuwainua kimaisha
Monday, 23 May 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment