Tuesday, 17 May 2011

POLISI WATATU MAHAKAMANI KWA KUOMBA RUSHWA

Polisi watatu mahakamani kwa kuomba rushwa

Na Jumbe Ismailly,Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Singida, imewapandisha kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Manyoni askari polisi watatu wa kituo mji mdogo wa Itigi, wilayani kwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni mbili.
Waliofikishwa katika mahakama hiyo ni pamoja na Joseph Raphael Nkurlah, Nasibu Thabiti Njovu na Noeli Madimo Philimon ambao hata hivyo nyadhifa pamoja na umri wa kila mmoja wao hazikuweza kupatikana mara moja.
Kwa mujibu wa mwanasheria wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Singida, Antidius Rutayuga, askari polisi hao wamefunguliwa kesi namba 81/2011 Machi 29, mwaka huu katika mahakama hiyo.
Aidha Mwanasheria huyo alisema mashitaka ya askari hao yapo chini ya vitendo vya rushwa k/f cha 15 (1)(a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa nambari 11/2007.
Rutayuga alisema kwamba, Januari 23 mwaka huu washitakiwa kwa pamoja wakiwa katika kijiji cha Kazikazi, tarafa ya Itigi wilayani humo waliomba na kushawishi wapewa rushwa na mzee Samson Ntungwa (68) shilingi milioni mbili ili wasimfungulie kesi ya kumficha muhalifu wa kesi ya mauaji aliyetambulika kwa jina la Mussa Bakari.
Kwa mujibu wa maelezo ya mwanasheria huyo siku ya tukio Januari 25, mwaka huu katika muda usiofahamika wakiwa kwenye kituo chao cha kazi washitakiwa hao kwa pamoja
walipokea rushwa ya shilingi milioni mbili tasilimu kutoka kwa mzee Samsoni.
Rutayuga kwamba washtakiwa hao kila mmoja kwa wakati wake walikana mashitaka hayo na wako nje kwa dhamana hadi Mei 19,mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.

No comments:

Post a Comment