Sunday, 8 May 2011

ASHTAKIWA KUVUNJA, KUIBA IKULU.

Ashitakiwa kuvunja, kuiba Ikulu

Na Khamis Amani
OFISI ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), imemfikisha mahakamani kijana wa miaka 23 akikabiliwa na shitaka la kuvunja nyumba ya makaazi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Pamoja na shitaka hilo, mshitakiwa huyo Mzee Khamis Mohammed anadaiwa kuiba mali inayokisiwa kuwa na thamani ya shilingi 1,500,000 mali ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pamoja na Ofisi hiyo ya DPP kumsomea mashitaka hayo mahakamani hapo, mshitakiwa huyo aliyakana na kudaiwa kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika.
Mshitakiwa huyo mkaazi wa Mpendae wilaya ya Mjini Unguja, alifikishwa mbele ya hakimu Omar Mcha Hamza wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kujibu mashitaka hayo.
Mara baada ya kukana mashitaka hayo, mahakama hiyo ilimwachilia kwa dhamana ya shilingi 100,000 za maandishi, pamoja na wadhamini wawili wenye vitambulisho waliotakiwa kusaini bondi ya shilingi 50,000 kila mmoja.
Mashitaka hayo dhidi yake yaliwasilishwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Khamis Jaffar Mfaume, Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi hiyo ya DPP.
Awali akiwa mahakamani hapo, Khamis Jaffar alimsomea mshitakiwa huyo shitaka la kuvunja nyumba mchana kwa dhamira ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 297 (1) (a) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Katika maelezo yake, Mei 2 mwaka huu mshitakiwa huyo alidai alivunja nyumba ya Rais na kuingia ndani kwa dhamira ya kutenda kosa kubwa la wizi.
Alidai kuwa, mara baada ya kuingia ndani humo mshitakiwa huyo aliiba mashine moja ya kushindilia kokoto isiyojulikana namba wala aina ya mashine hiyo yenye thamani ya shilingi 1,500,000 kwa kukisia mali ya SMZ.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo na Mwanasheria huyo wa serikali, tukio hilo la wizi ni kinyume na kifungu cha 274 (4) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.
Hati hiyo ilifahamisha kuwa, matukio yote hayo yalitokea Ikulu ya Migombani wilaya ya Mjini Unguja, majira ya saa 2:00 za asubuhi ambayo aliyakana.
Hivyo Mwanasheria huyo aliiomba mahakama hiyo kuliahirisha na kulipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa, pamoja na kutolewa kwa hati za wito kwa mashahidi.Hakimu Omar Mcha Hamza alikubaliana na hoja hizo, na kuliahirisha hadi Mei 17 mwaka huu kwa kusikilizwa na kuutaka upande huo wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

No comments:

Post a Comment