Monday, 23 May 2011

MAALIM SEIF AIOMBA NORWAY ISAIDIE MAENDELEO

Maalim Seif aiomba Norway isaidie maendeleo

Asema matarajio ya wananchi makubwa mno
Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ameiomba Norway, kuisaidia Zanzibar katika kukabiliana na changamoto za kimaendeleo, kiuchumi na kijamii zinazovikabili visiwa hivi.
Maalim Seif, alieleza hayo jana kwenye mazungumzo yake na Balozi Norway nchini Tanzania Inguun Klespsivi, huko ofisini kwake Migombani mjini hapa.
Alisema changamoto kubwa inayoikabili serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kitaifa, ni matarajio makubwa waliyonayo wananchi ya kupatikana haraka maendeleo na ustawishaji wa huduma za kijamii, huku uwezo wa serikali ukiwa hauwezi kukidhi haja hiyo kwa kipindi kifupi.
Alisema Zanzibar inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, hususan katika mkoa wa Mjini Magharibi, kutokana na miundombinu iliopo kuchakaa hali inayotia shaka usalama wa maji hayo pamoja na kumwagika ovyo.
Alisema mbali na msaada mkubwa kutoka Japan, kiasi cha shilingi milioni 163 zinahitajika ili kuondosha kabisa tatizo la maji safi na salama Unguja na Pemba.
Aidha alisema tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara kutoka Tanzania Bara kunakotokana na uchakavu wa waya wa baharini ni changamoto nyengine kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Hata hivyo Maalim Seif alimueleza Balozi huyo matumaini yaliopo kufikia ufumbuzi wa tatizo hilo kupitia mradi wa malengo ya Changamoto za Milenia (millennium challenge), hapo mwakani (2012).
Aidha Maalim Seif alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi huyo tatizo kubwa la ajira linalowakabili vijana na kuelezea mipango ya serikali katika kuwajengea uwezo na kuwawezesha kiuchumi.
Alisema serikali imeweka mkazo zaidi katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula na kupanda kwa bei za bidhaa hususan mchele, kwa kutumia ardhi ndogo iliopo kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo kiasi cha hekta 8,000 zimetengwa na pale lengo hilo litakapofikiwa tatizo hilo litakuwa limetatuka kwa asilimia 60.
Alisema serikali imeandaa mipango madhubuti ya kuwafunza wakulima juu ya matumizi bora ya ardhi, ili kupata kipato kikubwa na kuinua maisha yao.
Maalim Seif aliiomba Norway kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wavuvi wa Zanzibar, ambao wamekuwa wakiendelea kuvua kwa kutumia mbinu za kizamani na vifaa duni.
Aidha aligusia tatizo la magendo ya uvuvi wa bahari kuu, ambapo makampuni mbali mbali kutoka nchi za nje, ikiwemo Japan yanahusika na uhalifu huo.
Nae Balozi Klepsivik alisema Norway itaendeleza ushirikiano wake na Zanzibar kwa faida ya nchi hizo na wananchi wake.
Akizungumzia suala la uharamia unaofanywa na jamii ya Kisomali, alisema hili ni tatizo linaloikabili dunia, ikiwemo nchi za ukanda wa Mashariki na Kati ya Afrika.

No comments:

Post a Comment