Miaka 30 jela kwa kubaka mwanafunzi
Na Nalengo Daniel, Morogoro
MAHAKAMA ya Hakimu mkazi mkoa wa Morogoro imemuhukumu Hashimu Nunda (50) mkazi wa Kichangani Manispaa ya Morogoro kwenda jela miaka 30, viboko 12 na kulipa fidia ya Sh. 1milioni baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la kwanza.
Hukumu hiyo ilitolewa na hakimu wa Mahakama hiyo Maua Yusuph baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ambao haukuacha shaka yoyote katika kuthibitisha shitaka hilo.
Akisoma hukumu hiyo hakimu Yusuph alisema kuwa ametoa adhabu hiyo kali dhidi ya mshitakiwa ili iwe fundisho na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo ambayo aliiita kuwa ni ya kinyama ya udharirishaji.
Akijitetea ili mahakama impunguzie adhabu mshitakiwa huyo alidai kuwa anafamilia inayomtegemea wakiwemo wake zake wawili pamoja na wototo, ameshakuwa mtu mzima na pia ni mkosaji wa mara ya kwanza.
Hata hivyo hakimu huyo alitupilia mbali utetezi huo baada ya upande wa mashitaka kuiomba mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshitakiwa kwa madai kuwa vitendo vya ubakaji vinaongezeka kwa kasi na vimekuwa vikiwadharirisha hasa watoto na kuwaathiri kisaikolojia.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka Mrakibu msaidizi wa polisi Agostino George kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 20 mwaka huu saa 12: 55 jioni katika eneo la Kichangani Manispaa ya Morogoro.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa mshitakiwa akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa alimbaka mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka nane ambaye ni mwanafunzi anayesoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Mtawala baada ya kumlaghai na kumpeleka kwenye mashamba ya miwa ya Kichangani na kumbaka kisha kumsababishia maumivu makali.
Alipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza mshitakiwa huyo alikana shitaka na hivyo upande wa mashitaka ulilazimika kupeleka mashahidi ambao waliithibitishia mahakama pasipokuwa shaka yoyote kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kama alivyoshitakiwa mahakamani hapo.
Saturday, 14 May 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment