Friday, 6 May 2011

YAHAYA ARITHI MIKOBA YA RAVIA MAO DZENDOG

Yahaya arithi mikoba ya Ravia Mao Dzendog

Na Donisya Thomas
SIKU Chache baada ya Chama cha Soka Zanzibar ( ZFA), kumtimua aliyekuwa meneja wa uwanja wa Mao Dzedong, Ravia Idarous, hatimae ZFA imemtangaza Yahya Juma Ali, kuwa Meneja mpya wa uwanja huo.
Yahya ambae pia ni Katibu wa ZFA wilaya ya Mjini, anachukua nafasi hiyo baada ya ZFA Taifa kumtoa kafara Ravia, kutokana na msimamo wake wa kuupinga waziwazi uongozi huo.
Kwa mujibu wa barua ambayo Zanzibar Leo ilipata nakala yake inasema Yahya ameteuliwa kushika nafasi hiyo kuanzia Mei 5 mwaka huu.
Aidha barua hiyo ilielezea na majukumu yatakayofanywa na meneja huyo mpya kuwa ni pamoja na kuhakikisha usafi unadumishwa kiwanjani hapo, kuboresha na kusimamia maslahi ya wafanyakazi wa kiwanja hicho na kutoruhusu mtu, timu au taasisi yoyote kutumia kiwanja hicho bila idhini ya Katibu Mkuu wa ZFA Taifa.
Mbali na hayo, majukumu mengine aliyopangiwa ni kuhakikisha kiwanja hicho kinatumika vizuri na kwa nidhamu, kabla ya kufanya maamuzi ahakikishe anatoa ushauri kwa Katibu Mkuu wa ZFA Taifa pamoja na kufanya kazi nyengine atakayoelekezwa na Katibu Mkuu.
Alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi juu ya uteuzi huo Yahya, alisema ameshapokea barua kutoka ZFA iliyomtaarifu juu ya uteuzi huo na kwamba ameupokea kwa mikono miwili.
“ Ndio nimepata barua ya ZFA nipo tayari kufanya kazi hiyo mpya na ninaahidi kushirikiana vizuri na wakuu wangu”, alisema.
Kuhusiana na kumudu kazi mbili za Ukatibu wa ZFA wilaya ya Mjini na Umeneja wa Mao Dzedong, alisema, hayo yote ni majukumu ya kimichezo hivyo haitakuwa shida kwake kufanya kazi hizo kwa wakati mmoja.

No comments:

Post a Comment