Saturday 14 May 2011

UMEME WA JUA KUENDESHWA NA MAJI

Umeme wa jua kuendeshwa na maji

Na Zahor Suleiman
CHINA imekubali kuisaidia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kutumia teknolojia ya umeme wa jua ambayo itaendesha pampu za kusukumia, kuchimba visima na ulazaji wa mabomba ya maji safi na salama kwa vijiji vya Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Qiman alipokuwa akizungumza na waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ali Juma Shamuhuna huko ofisini kwake Shangani mjini Zanzibar.
Balozi huyo sambamba na msaada huo aliahidi Nchi yake pia kuisaidia Zanzibar katika kuipatia umeme wa teknogia hiyo kwa matumizi ya taa za barabarani kwa mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Balozi huyo alimueleza waziri Shamuhuna kwamba China itaisaidia Zanzibar katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na teknolojia ya habari kwa kuunganisha TVZ na matumizi ya mitambo hiyo ya umeme wa jua ili kuimarisha matangazo yake.
''Tunakusudia kuleta wataalamu wetu wa umeme huo wa jua kuendesha mitambo sambamba na wataalamu wa Zanzibar kupatiwa mafunzo ya muda mfupi nchini China kwa ajili ya kuendesha mitambo hiyo'', alisema Balozi huyo.
Nae waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Ali Juma Shamuhuna, aliishukuru Jamhuri ya Watu wa China kwa misaada yake mingi ya kimaendeleo kwa Zanzibar na kumuahidi Balozi huyo kutoa kila aina ya mashirikiano ili kuhakikisha mipango hiyo inafanikiwa na hatimae kuimarisha sekta hizo muhimu za maendeleo.
Mamlaka ya Maji Zanzibar inakabiliwa na changamoto mbali mbali za kuimarisha huduma za maji ikiwemo uchakavu wa mabomba na matumizi makubwa ya umeme wa kuendeshea pampu za kusukumia maji.
Zaidi ya visima vya maji safi na salama 49 vinavyohudumia Mkoa wa Mjini Magharibi pekee lakini bado upatikanaji wa huduma ya maji kwa baadhi ya maeneo ni kwa mgao.
Hali hiyo inasababishwa na kuharibika mara kwa mara kwa pampu za kusukuma maji kwa sababu mbali mbali za kiufundi pamoja na maji mengi kuvuja kutokana baadhi ya maeneo miundo mbinu ya kusambazia ni chakavu.

No comments:

Post a Comment