Tuesday, 10 May 2011

ZIARA BALOZI IDDI IRAN YAZIDISHA UHUSIANO.

Ziara Balozi Iddi Iran yazidisha uhusiano
Na Abdulla Kitole
ZIARA ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi   nchini Iran imezidi kuimarisha uhusioano uliopo baina ya nchi  hizo.
Balozi wa Iran nchini Tanzania Balozi Movahhedi Ghomi, alieeleza hayo alipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, yaliofanyika ofisini kwa Makamu huyo Vuga.
Balozi huyo alisema viongozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran walituma taarifa rasmi kwake juu ya kufurahishwa kwao na ziara hio ambapo walisema makubaliano mazuri yalifikiwa.
Alisema kuwa kufuatia makubaliano hayo kwa kuanzia tayari timu mbili za ujumbe kutoka Iran zinatarajiwa kuja Tanzania hivi karibuni, moja kuhusu Elimu na Vyuo vya Amali na nyengine kuhusu Kiwanda cha Utengenezaji wa Boti za Faiba.
Alieleza kuwa masuala mengine ni kuhusu miradi iliyokwama Tanzania Bara likiwemo suala la msaada wa matrekta ambapo kiasi ya matrekta 150 yanatarajiwa kupelekwa Tanzania Bara kwa ajili ya mradi wa kilimo kwanza na 50 kwa Zanzibar. 
Aidha, Balozi huyo alisema Makamu wa Rais wa Iran Dk. Mohammad Reza Rahimu ameeleza kuwa ziara hio imewezesha kufufua makubaliano kadhaa yaliokuwa yamekwama kwa upande wa Bara na Visiwani likiwemo suala la kuanzishwa kwa Ubalozi Mdogo wa Iran Zanzibar.
Akieleza shukrani zake kwa mafanikio hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema tayari timu ya wataalamu wa Zanzibar nayo imeshateuliwa kama ilivyoagizwa katika makubaliano yaliofikiwa huko Iran.
Aidha alieleza kufurahishwa kwake na hatua za Serikali ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran ya kuonesha nia yao njema ya kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo kwa hatua.

No comments:

Post a Comment