Monday, 23 May 2011

GLOBAL FUND YAISAIDIA BODI YA CHAKULA

Global Fund yaisaidia Bodi ya Chakula

Na Fatma Kassim, Maelezo
BODI ya Chakula, Dawa na Vipodozi imepata msaada wa vifaa mbali mbali vya uchunguzi kutoka shirika la mfuko wa Fedha wa Dunia Global Fund vyenye thamani ya shilingi 21,852,000.
Vifaa hivyo ni pamoja na mashine ya HPLC ambayo itatumika kwa ajili ya uchunguzi na ubora wa usalama wa Chakula Dawa na Vipodozi pamoja na ‘mini lab kits’ za kuchunguzia ubora wa dawa za binadamu, mifugo na kemikali mbali mbali za kimaabara.
Mrajis wa Bodi hiyo Dk. Burhan Othman Simai alisema kupatikana kwa vifaa hivyo kutaisaidia Bodi hiyo kufanya kazi zake kwa ufanisi na utaalamu.
Aidha alifahamisha kuwa vifaa hivyo vimekuja wakati muafaka ambapo Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar itashiriki katika uwiano wa usajili wa dawa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema katika uwiano wa usajili wa dawa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutasaidia katika kupunguza tatizo la dawa zisizosajiliwa pamoja zisizofaa kwa matumizi ya mwanadamu kwa nchi za Afrika Mashariki.
Dk. Burhan alisema Bodi yake itazidi kuhakikisha kuwa dawa bandia na duni haziingii nchini kwani zinaweza kuleta athari kwa mtumiaji, na shirika la Afya Ulimwenguni linapambana na dawa hizo hususan za kutibu maleria.
Katika hatua nyengine Bodi hiyo inatarajia kufanya uchunguzi wa kina juu ya kuwekwa madini joto kwenye chumvi inayotumiwa na wananchi.
Alisema uchunguzi huo utasaidia kutambua uwekwaji wa madini joto katika chumvi na kuepusha athari mbali mbali kwa chumvi ambayo haina madini joto ambayo ni pamoja na kuwa na watoto wasio na afya ya kutosha.

No comments:

Post a Comment