Friday 20 May 2011

WAFANYAKAZI USTAWI WA JAMII WASISITIZA KUONGEZA TAALUMA

Wafanyakazi ustawi wa jamii wasisitiza kuongeza taaluma

Na Sharifa Maulid
MKURUGENZI Idara ya Mipango, Sera na Utafiti wa wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto Mhaza Gharib Juma, amewataka wafanyakazi wa Ustawi wa Jamii kufanyakazi kwa umakini na kwa kutumia taaluma zinazohusu kazi zao.
Mkurugenzi huyo alieleza hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku nane kwa wafanyakazi 44 wa Idara ya Ustawi wa jamii wa Unguja na Pemba, yaliyoendeshwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii Dar-e-salaam na chuo cha jamii cha Jane Addams cha Illinois Chicago nchini Marekani.
Alisema wakati umefika wa kuwepo mabadiliko katika utendaji wao na mabadiliko hayo yatafanyika endapo wafanyakazi hao watatumia taaluma zao katika kuihudumia jamii.
Mhaza alisema ipo tofauti ya wafanyakazi wenye elimu na wale wanaofanyakazi kwa kutumia uzoefu huku akisisitiza wenye elimu watumie taaluma zao katika utoaji wa huduma.
Alisema ni muhimu kwa wafanyakazi hao kujitahidi kuiboresha jamii kwa kufuata mila na desturi za Zanzibar ili kuweza kuwatunza watoto na wazee. “Napenda kuwahakikishieni wawezeshaji kuwa Elimu mtayoitoa itatumika kwa maslahi na ustawi wa wananchi wa Zanzibar”, alisema.
Mkurugenzi huyo alilishukuru shirika la misaada la Marekani (USAID) kupitia asasi ya kimataifa American International Health Alliance (AIHA) kwa mchango wake ambao umewezesha kufanyika kwa mafunzo hayo.
Washiriki wa mafunzo hayo waliwashukuru wawezeshaji kwa njia walizotumia ambazo zimeweza kufahamika kwa wote na kuwaomba kutembelea katika sehemu za kazi baadae ili kuona utendaji wao.
Wamesema taaluma waliyoipata ya kushughulikia masuala ya kesi za watoto na namna ya kutatua kesi za kiustawi itawafanya kutekeleza majukumu yao vyema.

No comments:

Post a Comment