Tuesday 10 May 2011

SEMINA ELEKEZI YA VIONGOZI, WATENDAJI SERIKALI YA TANZANIA.

SEMINA ELEKEZI YA VIONGOZI, WATENDAJI SERIKALI YA TANZANIA

JK: Uongozi ni kutumikia wananchi

·        Ataka viongozi wa kisiasa, watendaji kushirikiana
·        Asema ulevi, uzinzi, rushwa si sifa ya kiongozi
·        Akemea Mawaziri, Makatibu Wakuu kuficha habari
·        Aeleza kuficha habari ni kukaribisha upotoshaji taarifa
·        Aagiza maofisa habari waruhusiwe kuzungumza
·        Ataka uwajibikaji kuongezwa kufikia Vision 2025
·        Asema mafanikio MKUKUTA 1 hayaridhishi
·        Nguvu zielekezwe kurekebisha kufanikisha MKUKUTA 2
·        Abainisha umasikini bado tatizo Tanzania
·        Ataka viongozi wasibweteke maofisini
·        Watembee kuona changamoto za maisha ya wananchi
·        Asema vita dhidi ya rushwa, dawa za kulevya kuendelea
·        Viongozi kuendelea kubanwa kimaadili
·        Ataka jitihada kukusanya mapato zaidi
·        Aagiza umakini kuongezwa kuziba mianya kuvuja mapato
·        Ataka huduma za jamii kuenezwa zaidi na kuboreshwa


Na Mwandishi wetu

VIONGOZI wa kisiasa na Watendaji wa Serikali ya Tanzania, wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo wakielewa kuwa kupewa kwao vyeo ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Hayo yalielezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Jakaya Mrisho Kikwete, alipofungua semina elekezi kwa viongozi hao Mjini Dodoma jana.

Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na vituo mbali mbali vya televisheni na redio na kushuhudiwa na waandishi wa vyombo vya habari mbali mbali nchini, ambapo gazeti hili limefuatilia kupitia vituo hivyo, Dk.Kikwete ameeleza kwamba uwajibikaji na ushirikiano wa viongozi wa kisiasa na watendaji wakuu ndiyo dira ya mafanikio na maendeleo ya nchi.

Dk.Kikwete aliwaeleza bayana viongozi hao kuwa ni lazima washirikiane ili wawe mfano wa kuigwa na wanaowaongoza huku wakielewa kuwa matumaini ya wananchi kwa Serikali yao yako katika majukumu waliyopewa wao.

Rais Kikwete aliwataka viongozi kuelewa kwamba mbali ya majukumu yao ya kikazi, pia wanalazimika kubadilika kitabia, kwani kuna baadhi ya mambo ni aibu kufanywa na viongozi wa juu Serikalini.

“Ulevi kupindukia mpaka unabebwa, uzinzi, ulaji rushwa na matusi mbele ya walio chini yako si sifa ya uongozi…….ni lazima tujiepushe na mambo hayo” alisisitiza Dk.Kikwete.

Dk. Kikwete alikemea tabia ya Mawaziri na Makatibu wakuu kukataa kutoa habari kwa vyombo vya habari nchini kuhusiana na mambo yanayohusu sekta zao, jambo ambalo husababisha upotoshwaji wa taarifa za Serikali na kukosesha wananchi fursa ya kuelewa utendaji halisi wa Serikali yao.

Kikwete aliwataka viongozi hao kuacha tabia ya kuwabana Maafisa habari wa Wizara, ambao wameajiriwa kwa lengo la kutoa habari, jambo linaweza kuwachochea kutoa habari kwa vyombo ambavyo mara zote vipo kutafuta habari hizo na baadae kuwalaumu kuwa wamepotosha.

“Mawaziri na Makatibu Wakuu mnawazuia Maafisa habari kutoa habari…….kila wakati mnataka mseme nyinyi na hapo hapo mnageuka ‘punching bag’” alieleza Rais Kikwete.

Akizungumzia umasikini nchini, Rais Kikwete amesema bado Watanzania walio wengi wanaishi maisha ya kimasikini ambapo Tanzania ni moja kati ya nchi 49 zilizo na umasikini mkubwa duniani, ambapo kupitia MKUKUTA 1 umasikini umepungua kwa asilimia 2 miaka mitano iliyopita.

Amesema katika kuongeza kasi ya kupunguza umasikini kuna haja ya hatua madhubuti kuchukuliwa kuhakikisha umasikini unaondoka zaidi kwa kurekebisha matatizo kupitia MKUKUTA 2.

Alisema juhudi zichukuliwe kufikia lengo la kuiwezesha Tanzania kuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoelezwa kwenye Dira ya Maendeleo ya 2025.

Akitaja baadhi ya njia za kuondosha umasikini nchini, Dk.Kikwete alisema ni kuinua hali za maisha ya wananchi kwa kuwaongezea kipato na kuwawezesha kulala pazuri, kula vizuri na kusomesha watoto wao.

Nyengine alisema ni kuimarisha miundombinu na kuweka mikakati ya kuongeza ajira ili kila mmoja aweze kufanya kazi na kupata kipato, kuimarisha huduma za kijamii kama vile elimu, afya, maji na umeme kwa kuisogeza karibu na wananchi na kuifanya kuwa bora zaidi.

Aliwaambia viongozi hao ni wajibu wa Serikali kuwapatia huduma bora za kijamii wananchi hivyo wanalazimika kupanga mikakati ya kuweza kufanikisha hilo kwa kila sekta kupanga mipango ya utekelezaji.

Hata hivyo alibainisha changamoto zinazoikabili Serikali katika kufanikisha hilo, ambapo alisema linategemea zaidi upatikanaji wa rasilimali fedha kwa Serikali na matumizi yake.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali alisema hali si mbaya kwa kufikia zaidi ya Shilingi bilioni 500 kwa mwezi kwa wastani, lakini bado kiwango hicho hakitoshi na uwezekano wa kukusanya zaidi upo hivyo hatua zichukuliwe.

Alieleza kuwa kuna kundi kubwa lenye wajibu wa kulipa kodi ambalo halijafikiwa, pamoja na kuchukuliwa hatua zaidi za kuziba mianya inayovujisha mapato ya Serikali.

Alieleza chanzo chengine cha mapato kuwa ni misaada na mikopo kutoka Jumuiya mbali mbali za kimataifa, pamoja na nchi marafiki, ambapo huko nyuma Tanzania imepata fedha nyingi kupitia vianzio hivyo na inatarajia kupata zaidi.

Akitoa mfano alisema tayari Benki ya Dunia imepanga kuipatia Tanzania dola bilioni 2.8 kama mkopo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Semina hiyo elekezi ambayo imeshirikisha Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi wa taasisi za umma na wakuu wa Mikoa na wilaya, imetoa maelekezo mbali mbali ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.

Miongoni mwa mada zilizotolewa kwenye semina hiyo ni masuala ya kuendeleza uchumi, mawasiliano ya habari kwa viongozi na wananchi, hali ya usalama wa Taifa, mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya.

Wataalamu wa ndani na nje ya nchi waliwasilisha mada hizo wakiwemo kutoka Benki ya Dunia, pamoja na viongozi wengine kuelezea uzoefu wao wa utendaji Serikalini akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa.

No comments:

Post a Comment