Saturday, 14 May 2011

VUAI AHIMIZA UWAJIBIKAJI CCM ZANZIBAR

Vuai ahimiza uwajibikaji CCM Zanzibar

Na Mwandishi Wetu
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali Vuai amewataka watendaji wa Chama hicho kutekeleza kwa vitendo maagizo ya halmashauri kuu ya taifa.
Vuai alieleza hayo jana ofisi kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa alipokutana na makatibu wa CCM wa mikoa, wilaya pamoja na maofisa wa chama wa ofisi kuu ya CCM Zanzibar.
Alisema ili chama kiimarike ni lazima washuke kwenye ngazi za chini katika ngazi ya shina, maskani na matawi ambako ndiko kwenye wanachama wengi wa chama hicho.
Alisema ili chama kisonge mbele katika kutekeleza majukumu yake ni lazima watendaji wa chama hicho wahakikishe wanafanya vikao kwa mujibu wa katiba.
Aidha Naibu huyo alisisitiza haja kwa viongozi hao kuhakikisha wanaandaa mikakati itakayosaidia kuanzisha miradi itakayokiwezesha chama kuongeza mapato ili kukimu gharama za uendeshaji.
Naibu huyo alitumia fursa ya mkutano huo kuwakumbusha viongozi hao kuwahimiza wanachama kulipa ada za uanachama na kuwa na moyo wa kutoa michango ya hiyari.
Alisema suala la maelewano na ushirikiano katika miongoni mwa watendaji nalo lina umuhimu wake na kusisitiza suala hilo kuendelezwa na kuepuka mifarakano.
Vuai alitoa wito kwa watendaji wa CCM wahakikishe wanafikia malengo ya kazi za kisiasa na kiuchumi mbele ya kamati za siasa.

No comments:

Post a Comment