Saturday, 14 May 2011

MAN UNITED MABINGWA WAPYA ENGLAND

Man. United mabingwa wapya England

LONDON, England
MANCHESTER United imetangazwa mabingwa wapya wa England, baada ya kulazimisha sare ya goli 1-1 na Blackburn Rovers kwenye dimbani la Ewood Park jana.
Sare hiyo iliiwezesha Manchester United kufikisha pointi 77 ambazo hazitaweza kufikiwa na waliokuwa wakishikilia taji hilo, Chelsea ambayo hata kama itashinda michezo yake miwili iliyobakia itafikisha pointi 76.
Chelsea leo itashuka kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Stamford Bridge kuikaribisha Newcastle United katika mchezo ambao utakuwa wa kusaka heshima na kuendelea kukaa katika nafasi ya pili.
Kipigo cha magoli 2-1 ilichokipata Chelsea dhidi ya Manchester United wiki iliyopita, kilifuta ndoto za miamba hiyo kuendelea kutetea taji hilo.
Manchester United sasa imebakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Blackpool kwenye uwanja wa Old Trafford ambao utakamalisha ligi hiyo Mei 22, kabla ya kuelekea katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona ya Hispania Mei 28, mwaka huu.
Blackburn iliwaweka roho juu mashabiki wa Manchester United kwa kufunga goli la kuongoza lililofungwa na Brett Emerton kunako dakika ya 20 huku mlinda mlango, Thomas Kuszczak, akienda sokoni.
Hata hivyo, Wayne Rooney, aliisawazishia Manchester United kwenye dakika ya 73 kutokana na mkwaju wa penalti na hivyo kushusha presha ya Sir Alex Ferguson.
Penalti hiyo ilitokana na mlinda mlango wa Blackburn, Paul Robinson, kumuangusha, Javier Herndandez, kwenye eneo la hatari na wageni kuzawadiwa penalti hiyo.
Kocha wa Manchester United, Sir Ferguson, aliwapongeza wachezaji wake kutokana na kujituma na kuweza kuibuka na ubingwa huo.
"Mchezo ulikuwa mgumu, lakini wachezaji walijituma na kupata pointi muhimu tuliyokuwa tukiihitaji", alieleza, Ferguson.
Huo ulikuwa ubingwa wa 19 kwa Manchester United na kuipiku Liverpool ambayo ilishatwaa ubingwa wa England mara 18.
Kwa matokeo hayo, Blackburn inaendelea kubakia kwenye nafasi ya 15 ikifikisha pointi 40 ambazo bado si salama kwa miamba hiyo katika janga la kushuka daraja.
Katika michezo mingine,Blackpool iliilaza Bolton magoli 4-3 huku Sunderland ikitandikwa magoli 3-1 na Wolves wakati West Brom iliilaza Everton goli 1-0.
Blackpool, Wigan na West Ham United zinaendelea kushika mkia wa ligi hiyo iliyobakisha mechi kukamilisha ratiba. (BBC Sports).

No comments:

Post a Comment