Friday 20 May 2011

WAWILI WASHIKILIWA KWA MAUAJI SINGIDA

Wawili washikiliwa kwa mauaji Singida

Na Jumbe Ismailly, Singida
JESHI la Polisi mkoani Singida linawashikilia watu wawili wa mji Mdogo wa Itigi, kwa tuhuma za kuharibu mali ya Benki ya NMB Tawi la Itigi na kumuua Juma Rashidi (32) mkazi wa Kijiji cha Tura, mkoani Tabora, aliyekuwa akituhumiwa kumuua dereva wa pikipiki (Bodaboda).
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Celina Kaluba aliwataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo kuwa ni pamoja na Mohamed Masudi (24) na David Nicodemu (25), ambapo tukio hilo lilitokea Mei 15 mwaka huu huko Itigi.
Kaluba alisema dereva huyo wa pikipiki alikatwa na kitu chenye ncha kali kisogoni na abiria huyo Geu Njongaji na kisha kudondoka chini na hatimaye kuchinjwa shingo kama kuku.
Kamanda huyo alibainisha kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kufanikisha mauaji hayo, aliamua kupora pikipiki hiyo yenye namba za usajili T.962 BNF aina ya Sanlag na kuiendesha kwenda hadi kwao katika Kijiji cha Tura.
"Inaelekea wazi kwamba baada ya kuipora pikipiki hiyo ndipo Geu aliiendesha kwa mwendo wa kasi na hata hivyo hakuweza kufika mbali, akaligonga shina la mti mkubwa na hivyo kuumia vibaya sana",alifafanua Kaluba.
Kamanda Kaluba alisema kutokana na majeraha aliyopata, ndipo Geu alipoamua kurudi tena Itigi kwa ajili ya kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Mtakatifu Gasper na ndipo wananchi waliokuwa wamepata taarifa ya kuuawa kwa dereva huyo wa bodaboda walimvamia na kuanza kumpa kipigo.
Alisema kamanda huyo kuwa hata hivyo licha ya uvamizi huo wa wananchi lakini inasemekana kwamba Geu aliweza kukimbilia katika Benki ya NMB Tawi la Itigi kwa lengo la kujisalimisha maisha yake, lakini kundi kubwa la wananchi wenye hasira
Kilimfuatilia nakufanikiwa kumtoa nje na kasha kumpiga kwa silaha mbalimbali na hivyo kusababisha kifo chake.
"Hata hivyo baada ya wananchi hao wenye hasira kukatazwa kuingia ndani ya majengo ya Benki na askari polisi waliokuwa lindo, ndipo waliamua kufanya fujo kubwa hadi kuharibu milango, madirisha, pamoja na vioo vya magari, hivyo
tunawashikilia Mohammed Masoud (24) na David Nicodemo (25) kuhusiana na mauaji na uhuribifu wa mali za Benki hiyo”, alisisitiza kamanda Kaluba.
Katika tukio jingine mkazi mmoja wa kijiji cha Ngimu, tarafa ya Mgori, katika halmashauri ya wilaya ya Singida, Raymond Erasto (26) aliwaua wazazi wake Erasto Kilakuno (78) na mama yake Frida Dule (57) kwa kuwakata kata kwa panga.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi wa Mkoa wa Singida, alisema mauaji hayo yamefanyika Mei 15 mwaka huu majira ya 1:45 jioni katika Kijiji cha Ngimu, tarafa ya Mgori na kwamba chanzo cha mauaji hayo inasadikiwa kwamba muuaji huyo alikuwa amerukwa na akili.
Aidha msemaji huyo wa jeshi la polisi alisema kuwa muda mfupi kabla kijana huyo kuwaua wazazi wake hao, alimjeruhi Ester Elihuruma (3) kwa kumkakata kwa panga sehemu mbali mbali za mwili wake na kumsababishia maumivu makali.
"Tayari tumeshamkamata mtuhumiwa huyo na bado tunakamilishe mambo machache yaliyobakia ili tuweze kumpeleka kwenye hospitali ya Mirembe, iliyoko Mkoani
Dodoma ili kwenda kuhakikiwa akili yake",alisisitiza kamanda Kaluba.

No comments:

Post a Comment