Tuesday, 10 May 2011

CHINA KUIUNGANISHA ZANZIBAR KIUTALII

China kuiunganisha Zanzibar kiutalii
Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya China inakusudia kulitumia eneo jipya la ushirikiano na serikali ya Zanzibar kwa kuhamasisha watalii wanaoingia nchini humo, kuvitembelea visiwa vya Zanzibar.
Balozi Mdogo wa China hapa Zanzibar, Chen Yiman, alieleza hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilahi Hassan Jihad, huko ofisini kwake Mnazi mmoja.
Balozi huyo, alisema serikali ya China, italiangalia eneo hilo ambalo ni jipya katika ushirikiano na Zanzibar kwa kuona inawahamasisha watalii na wananchi wa China kuja Zanzibar kuangalia vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
“Naamini wananchi wa China wengi watapenda kuja Zanzibar kwani tayari wapo wanaokwenda kutembea Ethiopia, Kenya, Zimbabwe na Tanzania hili ni eneo jipya kwa Zanzibar yenye vivutio vingi vya kitalii pamoja na utamaduni unaopendeza”, alisema Balozi huyo.
Alisema hivi sasa China imekuwa ikipokea wageni kutoka katika mataifa mbali mbali ambao huingia kwa shughuli za kitalii ambapo China itaweza kuwatumia wageni hao pia kuwahamasisha kuja Zanzibar kwa kutumia Ubalozi wa Tanzania uliopo nchini humo.
Balozi huyo alisema kuitumia sekta hiyo kwa serikali yake kutoa mchango wake ni muendelezo wa ushirikiano wa nchi hiyo kwa serikali ya Zanzibar kutokana na hapo awali kutoa mchango wake mkubwa katika sekta ya habari.
Alisema mchango wa nchi hiyo kwa wizara ya Habari utaendelea ambapo hivi karibuni serikali ya nchi hiyo iliweza kutiliana saini mkataba wa mtambo wa kurushia matangazo wa masafa mafupi.
Hata hivyo, balozi huyo pia alisema kuwa eneo jengine ambalo serikali yao italiangalia katika programu zake ni kuanzisha utoaji wa mafunzo kwa mafundi mitambo waliopo chini ya Wizara hiyo.
Nae waziri wa wizara hiyo, Abdilahi Jihad Hassan, alimshukuru Balozi huyo kwa kueleza kuwa dhamira ya serikali ya China kwa serikali ya Zanzibar ni sehemu itayoendeleza udugu kati ya nchi hizo ambao upo kwa muda mrefu.
Alisema nia ya China ni kuyaangalia maeneo mapya ya kuwekeza katika sekta ya Utalii hilo ni jambo la faraja kubwa baada ya serikali ya China kuitikia wito wa SMZ ambao uliiomba China kuitumia Zanzibar kuwekeza katika sekta hiyo ya utalii.
Kwa upande wake waziri Jihadi alisema nyanja hiyo ya mashirikiano itasaidia ongezeko la watalii wanaoingia hapa visiwani.
“Nimelifurahia hili, tulikwenda Takao kuna watalii wengi kama wakija Zanzibar itatusaidia kusukuma uchumi wetu kuna watalii wengi kutoka Urusi, Hungary, Croatia hawa bado soko lao hatujalikamata lakini kwa kupitia China tutaweza tukalikamata kwani leo hili kama samaki ameingia katika dema ndugu zetu China watatusaidia”, alisema waziri huyo.
Aidha waziri huyo alisema amefurahishwa suala la kupatiwa mafunzo watendaji wa Vyombo vya habari hasa sehemu ya ufundi, kwani hujitokeza matatizo ya kuharibika kwa mitambo mara kwa mara.
Serikali ya China imekuwa ikitoa misaada mbali mbali kwa serikali ya Zanzibar hasa katika sekta ya habari na Afya na maeneo mengine.
Wakati huo huo, serikali ya Misri imeitaka serikali ya Zanzibar iwe wazi kama wataalamu wanaoletwa na nchi hiyo hawafai.
Naibu Mhariri wa gazeti la  Misri, Hossam Diab wakati alipofanya mazungumzo na waziri Habari, Utamaduni Utalii na Michezo, Abdilahi Hassan Jihad, huko ofisini kwake Mnazimmoja mjini Zanzibar.
Diab alisema Misri kwa muda mrefu imekuwa na uhusiano na Zanzibar na huwapatia wataalamu wa fani mbali mbali kwa maendeleo ya Zanzibar lakini haitakuwa busara kwa serikali ya Zanzibar pale itapopatiwa wataalamu hao na kugundua kuwa hawafanyi kazi zao vizuri halafu ikikaendelea kunyamaza kimya.
Nae waziri Jihadi aliishukuru nchi hiyo kwa misaada inayoipatia Zanzibar na kuahidi kukuza ushirikiano ili kuona wanapata maendeleo zaidi na kukubali kuingia katika makubaliano ya kuipatia programu kwa vituo vya  habari vya hapa nchini.

No comments:

Post a Comment