Tuesday, 3 May 2011

DK. SHEIN AWATAKA WAWEKEZAJI WA UTURUKI KUWEKEZA ZANZIBAR.

Dk.Shein awataka wawekezaji wa Uturuki kuwekeza Zanzibar

• Awambia mazingira, miundombinu inavutia
• ZIPA yafafanua mipango iliyowekwa
Na Rajab Mkasaba, Uturuki
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa wito kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini Uturuki kuweka vitega uchumi vyao Zanzibar ikiwa ni njia mojawapo kuinua uchumi na kuimarisha mahusiano baina ya pande mbili hizo.
Akizungumza katika mkutano maalum na wawekezaji na wafanyabiashara katika mji wa Istambul nchini Uturuki jana, Dk. Shein amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeimarisha Sera za uwekezaji Zanzibar ili kupunguza usumbufu na kuwavutia zaidi wawekezaji kutoka maeneo mbali mbali duniani.
Dk. Shein ambaye amemaliza ziara yake inayotokana na mwaliko wa Rais wa Uturuki, Abdallah Gul, amesema Benki ya Dunia imeipa nafasi ya pili Zanzibar kati ya nchi 37 zenye uchumi unaofanana katika kurahisisha taratibu za uwekezaji ambapo nchi ya kwanza ni Singapore.
Amesema hatua hiyo inathibitisha utayari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutoa huduma kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Zanzibar.
Ameongeza kuwa ili kuhakikisha taratibu za kuwekeza zinafanywa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi, serikali imeunda Mamlaka ya Vitega Uchumi (ZIPA) ambayo inashughulikia masuala ya uwekezaji Zanzibar.
Aidha, Dk.Shein amesema Zanzibar inayo maeneo mengi ya kuwekeza hasa kwenye sekta ya utalii kutokana na utamaduni wa nchi hiyo unaofanana na Uturuki.
Alisema idadi ya watalii wanaoitembelea Zanzibar kutoka bara la Ulaya imekuwa ikiongezeka kila mwaka na mahitaji ya hoteli na huduma nyengine yamekuwa yakiongezeka sambamba na mahitaji zaidi ya watalii hao.
Alisisitiza kuwa hadi sasa Zanzibar kuna hoteli 225 tu pamoja na nyumba za kulala wageni ambazo zinafanya jumla ya vyumba 5301. Amesema mashirika mbali mbali ya ndege yanatoa huduma kwa watalii wanaotembelea Zanzibar lakini alieleza haja ya wawekezaji wa Uturuki kuangalia uwezekano wa kuongeza safari za ndege kati ya Zanzibar na Jimbo la Utalii la Antalya ambalo linachukua idadi kubwa ya watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Akizungumzia maeneo mengine ya uwekezaji, Dk. Shein alisema kuwa zaidi ya utalii, wawekezaji wanayo nafasi kubwa ya kuwekeza katika maeneo ya uvuvi pamoja na viwanda vidogo vidogo vinavyotokana na rasilimali zilizopo Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein amesema Zanzibar inayo fursa ya kushirikiana kiuchumi na kibiashara kwa kutumia bandari yake iliyopo na kuwa na uwezo wa kupitisha bidhaa kutoka Mashariki ya Kati na Ulaya.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wawekezaji hao kuwa pia, wanaweza kuwekeza katika sekta ya elimu na huduma za afya hasa katika elimu ya juu.
Akitoa maelezo juu ya juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wafanyabiashara na wawekezaji hao Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum Khamis Nassor alisema kuwa Sera ya uwekezaji Zanzibar imeanzishwa ili kutoa maelekezo kwa taasisi za serikali kwa lengo la kukaribisha wawekezaji kutoka sekta binafsi ili iweze kuchangia ukuaji wa uchumi Zanzibar.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa (ZIPA) imepewa jukumu la kusimamia uwezeshaji wa utekelezaji wa miradi ya kiuchumi bila ya urasimu.
Alisema hadi kufikia Disemba 2010 ZIPA imeidhinisha utekelezaji wa miradi 444 katika sekta mbali mbali, ambapo kati ya hiyo 282 inajishughulisha na biashara ya utalii katika nyanja mbali mbali.
Aliendelea kueleza kuwa wawekezaji wanaendelea kukaribishwa Zanzibar ikiwemo seka ya uvuvi wa bahari kuu, ili rasilimali za bahari ziweze kunufaisha uchumi wa Zanzibar.
Aidha, alisema katika sekta ya kilimo wawekezaji wanakaribishwa kujikita katika kilimo cha mbogamboga kwa kutumia taaluma ya kisasa (Green House) hasa kwa kuzingatia uhaba wa ardhi ya Zanzibar.
Hata hivyo, alieleza kuwa msisitizo pia, umewekwa kwamba ardhi ya uwanda inaweza kutumika kwa kilimo kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Mkurugenzi huyo pia, alitaja maeneo mengine katika sekta ya utalii ambayo ni uwekezaji wa mahoteli makubwa ya kuanzia nyota tano. Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa ujenzi wa nyumba za biashara katika maeneo huru ya kiuchumi ambao utaenda sambamba na uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo na vya kati vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hasa matunda na mazao mengine ya kilimo.
Nao wawekezaji na wafanyabiashara wa kupitia Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Uturuki (TUSKON) wameeleza nia yao ya kuwekeza Zanzibar na kupongeza mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uwekezaji na biashara ikiwemo Sera yake madhubuti.
Aidha, walieleza pia, kuvutiwa zaidi katika miradi ya miundombinu kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ‘Puplic Private Partnership’(PPP).
Pamoja na hayo, wafanyabiasahara na wawekezaji hao wamesifu na kueleza kuwa kuwepo kwa amani na utulivu Zanzibar kutawavutia zaidi kuja kuwekeza katika sekta mbali mbali za maendeleo haraka iwezekanavyo.
Dk. Shein na ujumbe wake wamerejea nchini jana baada ya kumaliza ziara yake hiyo.

No comments:

Post a Comment