Wapongeza mpango wa kukomesha maji Mnazimmoja
Washauri agizo la Rais lipewe kipaumbele
Na Salum Vuai, Maelezo
WAPENDA michezo mbalimbali wa Zanzibar, wamepongeza hatua ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kutaka jitihada zifanywe kurekebisha miundombinu ya uwanja wa Mnazimmoja ili kumaliza tatizo la kutuwama maji.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tafauti, baadhi ya wananchi wamesema iwapo kauli ya Rais itafanyiwa kazi na kuurejesha uwanja huo katika hali ya kuweza kutumika kwa vipindi vyote, itakuwa faraja kubwa kwa wanamichezo wanaotumia uwanja huo kwa mazoezi.
Mkurugenzi wa klabu ya Miembeni Haji Sultan 'Kaka', amesema miundombinu mibovu inayoufanya uwanja huo kutuwama maji kila msimu wa mvua unapofika, inawanyima vijana fursa ya kuendeleza programu za mazoezi wanazojipangia, na hivyo kushusha viwango vyao vya soka.
"Kwa mfano sasa ni wakati wa masika, maji ambayo hayawezi kutolewa yamejaa, inatubidi tutafute viwanja mbadala vya mazoezi ambavyo havipo huku tukikabiliwa na mechi za ligi", alisema Sultan ambaye klabu yake inayoshiriki ligi kuu inatumia sehemu ya uwanja huo kwa mazoezi.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa ZFA Wilaya ya Mjini Nassor Salim Ali 'Jazeera' ambaye pia ni Mwakilishi wa jimbo la Rahaleo, amepongeza hatua ya Rais kuzipigia upatu mamlaka zinazohusika kuufanyia matengenezo uwanja huo, akisema hatua hiyo itawaondoshea usumbufu wanasoka wanaoutumia.
"Masika yanapokuja huchukua muda mrefu, kipindi chote hicho kinawafanya wanasoka wavunde kwa kukosa mazoezi, kauli ya Mheshimwa Rais ni ya kupongezwa na tunaamini wahusika wataifanyia kazi haraka kwa sababu tunafahamu uwezo wa kurekebisha uwanja huu upo", alisema Jazeera aliyekutwa karibu na uwanja huo kwa shughuli maalumu.
Naye Abdul Mshangama ambaye ni mchezaji mwandamizi wa timu ya Wazee Sports, amesema Dk. Shein ameonesha kuguswa na maendeleo ya soka nchini, na kwamba agizo lake linaonesha namna anavyopenda vijana waendelezwe kimichezo.
Kwa miaka mingi, uwanja wa Mnazimmoja unashinda kutumika kila yanapofika majira ya mvua, kutokana na kujaa maji na kutuwama kwa muda mrefu huku wachezaji wengi wakijipa likizo za muda, ambapo Dk. Shein aliutembelea katika ziara yake ya Mkoa wa Mjini Magharibi hivi karibuni.
Monday, 23 May 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment