Friday, 6 May 2011

TASWA KUWAZAWADIA WANAMICHEZO LEO

TASWA kuwazawadia wanamichezo leo

Na Aboud Mahmoud
MCHEZAJI bora wa soka wa Zanzibar mwaka jana ambae pia huchezea timu ya Zanzibar Ocean View, Khamis Mcha 'Viali' ni miongoni mwa wanamichezo wanaotajwa kuibuka na gari katika hafla ya wanamichezo bora wa mwaka.
Hafla hiyo inayofanyika kila mwaka ambayo inaandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), imepangwa kufanyika leo katika hoteli ya Moven Pick jijini Dar es Salaam.
Mbali na Viali ambae pia huchezea timu ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' wengine ni walio katika mchuano huo mkali ni pamoja na Mrisho Ngasa (Azam), Shadrack Nsajigwa (Yanga) na Juma Kaseja (Simba).
Taarifa ya TASWA ilieleza tuzo ya heshima kwa kawaida huwa maalum kwa mchezaji aliyetoa mchango wake katika kuendeleza medani ya michezo nchini ambayo itatangazwa leo katika kilele cha hafla hiyo.
Wengine watakaozawadiwa tuzo ni wanariadha wanawake na wanaume, mpira wa wavu, netiboli, kareti, ngumi, gofu, kriket, judo na pia Watanzania wanaocheza michezo mbalimbali nje ya nchi.
Mratibu wa TASWA Zanzibar, Maulid Hamad Maulid, alisema, ni wanamichezo wawili watakaoshiriki katika hafla hiyo ambao ni Viali na Masoud Amour wa mchezo wa judo.
“Awali wachezaji watano wa Zanzibar tulikubaliwa tuwapeleke wote, lakini ghafla jana walitwambia watakwenda wawili kuwakilisha wenzao”, alisema, Maulid.
Hata hivyo, Maulid, ambae pia ni miongoni mwa watakaoshiriki katika hafla hiyo alisema, ataandaa utaratibu mwengine wa kufanya hafla fupi ya kukabidhi tuzo za waliosalia hapa Zanzibar.
Aliwataja nyota hao kutoka Zanzibar ni pamoja na Miza Nyange (netiboli), Ally Juma na Abdusamad Alawi (judo).
Alisema, kimsingi aliomba nafasi 10 kwa wanamichezo bora wa Zanzibar kuwakilisha michezo mbalimbali, lakini zikapatikana nafasi tano kwa vile hapo awali hawakupanga kuzawadiwa wanamichezo wa visiwani.

No comments:

Post a Comment