Ufaransa yaisaidia sekta ya maji Tanzania
Na Tiganya Vincent-MAELEZO-Dar es salaam
SHIRIKA la maendeleo la nchini Ufaransa (AFD) limetoa msaada wa msaada wa shilingi bilioni 1.2 (sawa na Euro 500,000) kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya maji hapa nchini Tanzania.
Msaada huo ulitolewa jana jijini Dar es salaam na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Jacques Champagne de Labriolle kwenye hafla fupi ya kusaini msaada huo zilizofanyika katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Uchumi ya Tanzania.
Balozi huyo alisema kuwa msaada huo unahusu kusaidia masuala ya kiufundi katika kuendeleza mpango wa maendeleo ya sekta ya maji katika miradi inayofadhiliwa na wahisani mbalimbali likiwemo Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD).
Alisema madhumuni ya mpango wa kuendeleza sekta ya maji (WSDP) ni kupunguza kiwango cha umasikini kwa kuwawezesha wananchi wengi kupata maji safi na salama yanayozingatia viwango vya ubora wa afya na mazingira.
Balozi huyo aliongeza kuwa kupitia mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa Tanzania (MKUKUTA), unaweka mkazo juu ya huduma ya maji na udhibiti wa sekta hiyo katika kufikia malengo ya milenia ambayo ni kupunguza idadi ya watu wasio na maji safi kwa kiwango cha nusu ifikapo mwaka 2011.
Balozi Labriolle alisema kuwa AFD inampango wa kusaidia miradi ya maji katika miji ya Bukoba na Musoma ambayo inatarajia kuanza mwanzoni mwa mwaka ujao na kuongeza kuwa mchango wa AFD kwenye kapu la sekta ya maji hivi sasa ni Euro milioni 30 sawa na shilingi bilioni 52.5.
Alifahamisha kuwa AFD imejipanga kusaidia utunzaji wa mazingiara ya Ziwa Victoria ambalo linakabiliwa na madhara yanayotokana na ongezeko la idadi ya watu katika maeneo ya Mwanza, Kisumu na Jinja.
Alisema kuwa misaada ya Ufaransa katika sekta ya maji safi na taka na usafi wa mazingira ni sehemu ya mpango mzima wa kuendeleza miundo mbinu ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania na nyingine za Afrika Mashiriki.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Ramadhan Khijjah alisema kuwa bado wananchi wote hawajapata maji safi na salama , hivyo msaada huo utasaidia kuendeleza kasi ya Serikali ya Tanzania kuhakikisha wananchi wengi wanapata maji safi na salama ifikapo 2025.
Alisema kuwa bila maji safi na salama maendeleo yanataendelea polepole na hivyo kusababisha uwepo wa matatizo mbalimbali ambayo yatasababishwa na mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayotokana na ukosefu wa maji.
Friday, 6 May 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment