Saturday, 14 May 2011

MAONI AJALI

Tuzikomeshe ajali za barabarani

AJALI za barabarani zimekuwa zikiongezeka ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopo kiasi cha watu 100 hufariki kila mwaka kutokana na ajali hizo ambazo hutokea sehemu mbali mbali nchini.
Hizo ni takwimu za vifo, lakini katika ajali hizo pia itegemewe kuwepo kwa majeruhi ambao wengine masikini hupata ulemavu wa kudumu bila ya kutegemea katika maisha yao, kweli kama hujafa hujaumbika.
Ajali zinazotokea huchangiwa kutokea kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo uzembe watumiaji barabara na uzembe wa madereva na hili linatokena na kutoeleweka kwa sheria za barabarani.
Tunakubali wapo watembea kwa miguu au waendesha vyombo vya magurudumu mawili baadhi yao hufanya uzembe na kusababisha ajali, lakini kwa kiasi kikubwa uzembe wa madereva wa gari ndio unaomaliza maisha ya wananachi.
Uzembe wa madereva hutokana na sababu mbali mbali ikiwemo wakati mwengine ulevi pamoja na shetani aliowajaa vijana ambaye huwasimamia na kuwaambia waendesha mbio vyombo hivyo.
Utashangaa vyombo vya moto kama vile pikipiki na vespa vinaendeshwa kwa mwendo wa kasi chochoroni na ikitokezea ajali ya kumgonga mtoto utasikua si makusudi.
Haikatazwi kuendesha vyombo katika mitaa yetu, lakini kwa spidi kama ya barabarani, hali unajua kuwa kutwa nzima watoto wanakwatisha njia wakiwa kwenye michezo yao.
Ajali zinazosababishwa na daladala hizo ndio hazisemeki ni za kizembe, uzembe ambao huwezi kukadiria kama unaweza kufanywa na dereva aliyefanyiwa majaribio kabla ya kupewa leseni.
Wapo madereva ambao kila siku wao wamekuwa wakikiuka sheria za barabarani hata haieleweki vigezo gani vilitumika kupewa lesini watu hawa.
Lakini wapo baadhi ya madereva walioua kwa kusababisha ajali wanaonekana mitaani wakidunda kama vile roho iliyotoka si ya binaadamu.
Suala hili ndilo linapa shida wananchi na kujiuliza, hivi hizi sheria zetu zikoje, mbona badala kulinda waliofanyiwa makosa zinawalinda waliofanya makosa.
Sisi tungependa kuona hatua zinachukuliwa katika kukabiliana na suala la ajali za barabarani ili kupunguza vifo vya watu pamoja na kupata ulemavu usiotarajiwa.
Bila shaka hilo litawezekana kama wale madereva watukutu watalazimishwa kutumia sheria za usalama barabarani.
Tunadhani hatua ya Idara ya Leseni na Usafiri ya kuwafutia leseni madereva watukutu ni miongoni mwa njia zitakazo weza kuwafanya madereva wa aina hii kufuata sheria za usalama barabarani.
Jambo jengine ambalo litaweza kupunguza ajali za barabarani ni sheria kwa dereva anayeua zirekebishwe na apewe adhabu kali.
Kwa njia hii kila dereva akishika usukani atakumbuka kuwa akiua sheria kali inamsubiri, hivyo tahadhari itakuwa kichwani mwake kila wakati kabla ya kusababisha ajali.

No comments:

Post a Comment