Monday, 9 May 2011

DK. SHEIN AWATAKA VIONGOZI SMZ KUACHA UHAFIDHUNA.

Dk. Shein awataka viongozi SMZ kuacha uhafidhina

• Ataka wabadilike kwa maendeleo, faida ya wananchi
• Awataka wazungumze na vyombo vya habari
• Aeleza matumaini Serikali yake kufanikiwa
Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amefunga semina ya siku tatu ya viongozi na watendaji wakuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusisitiza haja ya viongozi kubadilika katika suala zima la utendaji wa kazi kwa manufaa ya nchi na wananchi kwa jumla.
Katika maelezo yake mafupi ya ufungaji wa semina hiyo, iliyofanyika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Dk. Shein alieleza kuwa katika suala zima la kubadilika katika uongozi ni vizuri wakaanza viongozi hao wakuu ili iwe ni kigezo kwa wale wanaowaongoza.
Dk. Shein alieleza matumaini yake makubwa ya kufikia lengo lililokusudiwa kutokana na yale yote yaliyoamuliwa na kujadiliwa katika semina hiyo ya viongozi ambayo yanahitaji kutekelezwa.
Alisema kuwa uongozi ni kuongoza njia, iwapo viongozi watatekeleza vyema majukumu yao na kufanya kazi kwa bidii na ukweli mafanikio makubwa yatapatikana.
Dk. Shein alitoa shukurani kwa watoaji mada wote, washiriki pamoja na Sekretariati ya Jumuiya ya Madola yenye Makao Makuu yake Mjini London Uingereza kwa kusaidia ufanikishaji wa semina hiyo.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd kwa kushiriki kikamilifu katika semina hiyo pamoja na viongozi na watendaji wengine wakuu wa SMZ.
Mapema akitoa mchango wake katika mada ya Mawasiliano na Maendeleo iliyotolewa na Manoh Esipisu kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola ambayo ndiyo ilikuwa mada ya mwisho katika semina hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa viongozi wana wajibu wa kutoa taarifa za maendeleo kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Dk. Shein alieleza viongozi ni lazima wawe karibu na vyombo vya habari kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii sambamba na kuandaa utaratibu wa kuzungumza na vyombo hivyo kwa madhumuni ya kuwaeleza wananchi mandeleo yanayofikiwa nchini.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka viongozi hao kujiandaa katika kutoa taarifa kwa waandishi wa habari wa vyombo vya serikali na vile vya binafsi ili wananchi waelewe na wajue viongozi wao wanasema nini.
Katika semina hiyo, Dk. Shein alisisitiza mashirikiano ya pamoja kwa viongozi na watendaji wakuu wa serikali katika kuendeleza maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Akitoa michango yake katika mada mbali mbali zilizowasilishwa katika semina hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na mipango na mikakati madhubuti iliyowekwa na serikali anayoiongoza ana matumaini makubwa ya kufikia malengo yaliyowekwa na kupata maendeleo zaidi.
Aidha, washiriki wa semina hiyo nao walisisitiza haja ya waandishi na vyombo vya habari kutoa habari zilizo sahihi kama wanavyoelezwa na vyanzo vya habari wanazozipata wakiwemo viongozi hao wakuu wa serikali ambao waliahidi mashirikiano makubwa kwa waandishi wa habari kwa ajili ya maslahi na maendeleo ya nchi.
Nae mtoa mada juu ya mawasiliano na maendeleo alieleza umuhimu wa viongozi na watendaji wakuu wa serikali kuonesha mashirikiano yao kwa vyombo vya habari sambamba na kueleza mafanikio na maendeleo ya nchi kwa wananchi ili wapate uelewa mzuri juu ya hatua zinazochukuliwa na viongozi wao.
Mada mbali mbali zilitolewa katika semina hiyo ya siku tatu ambazo zimewapa uelewa mkubwa viongozi hao na watendaji wakuu wa serikali juu ya misingi ya uhusiano na mbinu za kukuza uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa kisiasa na watendaji wakuu katika kutekeleza majukumu ya viongozi kwa ufanisi zaidi.
Pia, wamepata kuelewa misingi ya uongozi, maadili na uwajibikaji na umuhimu wake katika utekelezaji wa majukumu waliyokabidhiwa kutokana na mada zilizotolewa.
Viongozi hao pia waliahidi kushirikiana kwa karibu zaidi na kuelekeza majukumu yao kikamilifu kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo endelevu.
Aidha viongozi hao walipata fursa ya kufahamu misingi muhimu ya itifaki na diplomasia na umuhimu wake katika utekelezaji wa shughuli za viongozi za kila siku pamoja na kujua hali halisi ya uchumi, mbinu na mikakati makhsusi ya kuimarisha uchumi pamoja na mambo mengineyo.

No comments:

Post a Comment