Machafuko Uarabuni yaongeza mfumko wa bei
Na Jumbe Ismailly, Iramba
KATIBU wa Uchumi na Fedha Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Lameck Nchemba Mwigulu amesema machafuko katika nchi za kiarabu yamechangia kupanda kwa gharama za maisha.
Mwigulu alisema hayo kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara aliyohutubia katika vijiji vya Makunda na Nkinto, wilayani hapa wakati wa ziara ya siku tano ya kuitambulisha sekretarieti mpya wa chama hicho.
Alisema machafuko yanayoambatana na maandamano katika baadhi ya nchi za kiarabu yamepandisha gharama za maisha huku kupanda kwa bei ya mafuta kukichangia mfumko wa bei na kupanda kwa gharama hizo.
Mwigulu ambaye ni Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi (CCM), alisema duniani kote maandamano huwa hayana faida zaidi ya kuongeza gharama za maisha kwa wananchi.
Alisema maandamano yanayoongozwa kila kukicha na viongozi wakuu wa Chama cha CHADEMA, nayo yamekuwa yakichangia kwa namna moja au nyingine gharama za maisha kutokana na watu kutumia muda wao mwingi kwenye maandamano badala ya kujikita kwenye uzalishaji.
“Kiongozi wao anayewaongoza nilimuhurumia sikujua kwa nini anafanya hivyo, lakini nikagundua ni dokta, hata nyie mtadhani ni dokta wa kweli, kumbe ni dokta wa sheria za kanisa, hajui yanayoendelea hapa”, alisema Mweka hazina huyo.
Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Oganaizesheni Asha Juma Juma, alisema sasa chama kimefuta utaratibu wa kuingiza wanachama wapya wa papo kwa papo kwa kuhofia vurugu zinazokuja kujitokeza mara tu baada ya kuwaingiza ndani ya chama.
Friday, 20 May 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment