Tutalirejeshea hadhi bonde la Cheju – Dk. Shein
Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali anayoiongoza italiimarisha bonde la Cheju kwa kuliwekea miundombinu bora ili lirejee kwenye historia yake ya kuzalisha mpunga kwa wingi.
Dk. Shein alieleza hayo jana kwenye ziara yake ya wilaya ya Kati, ambapo alisema serikali itaendelea na malengo yake ya kufanyia mapinduzi kilimo ikiwa ni pamoja na kuwashirikiana na kuwasaidia wakulima kikamilifu.
Alisema ahadi zote alizozitoa wakati wa kampeni ambazo baadhi zimeanza kutekelezwa, zilikuwa ni za ukweli na zitawasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi na wakulima wa bonde la Cheju.
Alifahamisha kuwa kilimo kinaweza kuimarika iwapo kutakuwepo kwa mbegu bora, mbolea, maji na utaalamu ambapo juhudi zitachukuliwa katika kuhakikisha wakulima wanapatiwa nyenzo hizo.
Dk. Shein alieleza kuwa serikali inaimarisha nguvu na kuwataka wakulima wasivunjike moyo na kuwahakikishia kuwa ndani ya miaka mitano sekta ya kilimo itabadilika.
Kwa upande wake Naibu waziri wa wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Issa Haji Ussi aliwahakikishia wananchi wa Cheju kuwa barabara yao kutoka Jendele hadi Unguja Ukuu imo katika mradi wa ujenzi ndani ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha ambao utaanza mwezi Julai.
Kwa upande wa huduma ya umeme, alisema umeshafikishwa katika bonde chini ya ushirikiano wa mradi wa PADEP ambao mashimo ya kusimamisha nguzo yameshachimbwa ambapo wakati wowote nguzo hizo zitawekwa yatawekwa kwa lengo la kupeleka huduma hiyo majumbani.
Nao wakulima wa Bonde la Cheju walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa juhudi zake alizozichukua za kuwatembelea na kusikiliza changamoto wanazozikabili pamoja na mafanikio makubwa waliyoyapata mwaka huu ambayo hayajawahi kutokea ndani ya miaka 15.
Katika ziara hiyo, alipokea taarifa ya mkoa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mustafa Ibrahim ambapo alieleza mafanikio yaliopatikana katika Mkoa huo pamoja na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa pamoja na changamoto zilizopo.
Baada ya taarifa hiyo ilianza kulitembelea Daraja la Mwera ambalo linaendelea na ujenzi ulioanza rasmi mwezi Januari mwaka huu ambalo linatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi wa Septemba ambapo ujenzi wa daraja hilo utagharimu shilingi bilioni 1.3.
Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano Dk. Idd Lila na kampuni ya ujenzi wa daraja hilo, walieleza kuwa daraja hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kupitisha magari yenye uzito hadi wa tani 160 kwa magari yenye line nne za matairi(4Axles),
Alisema daraja la zamani lililojengwa mwaka 1904 ambalo lilikuwa na uwezo wa kubeba tani 50 tu lilipokuwa jipya na sasa lina uwezo wa kubeba tani 5 kutokana na kuchakaa.
Akiwa katika shamba la kuku wa mayai Ubago, Dk. Shein alieleza haja ya kutolewa elimu kwa wafugaji wa kuku na kuelewa kuwa bado wapo wafugaji na wasambazaji wa kuku wazalendo ambao wanauwezo wa kuzalisha vifaranga na kuwauzia wafugaji hapa hapa Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein alizitembelea ujenzi wa skuli za sekondari za Wilaya ya Kati ikiwemo ile ya Uzini na ile ya iliyopo Jumbi ambapo zote hizo zinatarajiwa ujenzi wake kukamilika ndani ya mwaka huu na kuangalia ujenzi wa ofisi ya mkoa wa Kusini Unguja.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitembelea shamba la kuoteshea mbegu lililopo Bambi pamoja na shamba la JKU la mbogamboga na kupata maelezo juu ya uendelezaji wa mbegu mbali mbali ikiwemo mbegu ya mpunga ya Merica ambayo inachukua muda wa siku 90.
Monday, 23 May 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment