Friday, 17 June 2011

SMZ KUTEKELEZA MIRADI 77, PROGRAM 27.

SMZ kutekeleza miradi 77, programu 27• Yatenga 126.15 kulipa mishahara, uchumi kukuwa 7.9 %
Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema pato la taifa linatarajiwa kukua kwa kasi zaidi kutoka ukuaji wa asilimia 6.5 hadi kufikia asilimia 7.9 kwa mwaka 2011/2012.
Hayo yalibainika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi huko Chukwani nje kidogo wa mji wa Zanzibar, wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee wakati aliwapowasilisha mpango wa maendeleo na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Alisema ukuaji wa pato la taifa linatokana na matokeo ya kuimarika kwa miundombinu ya kiuchumi kama vile uwanja wa ndege, barabara, umeme na mfumo wa umwagiliaji maji pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji.
Sambamba na juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, ambazo zitaongeza kigavi cha mapato na kufikia asilimia 20.2 kutoka asilimilia 18 mwaka 2010/2011, ambapo alikumbusha kwamba uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 4.4 kwa mwaka 2011.
Alieleza kwa nchi zilizoendelea unatarajiwa kufikia asilimia 2.5 wakati nchi zinazoendelea na zilizo chini kiuchumi zinatarajiwa kukua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.5 kwa mwaka 2011 na nchi za Jangwa la Sahara zinaendelea kurejea katika hali ya kawaida kutoka katika msukosuko wa kiuchumi na fedha na matarajio ya ukuaji wa asilimia 5.5.
Alieleza Serikali imeazimia kujenga mazingira ya kiuchumi katika kuimarisha rasilimali watu, kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi, kuinua kiwango cha sayansi na teknolojia na mafunzo ya vitendo pamoja na kutekeleza mkakati wa usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.
Aidha alisema kwa mwaka wa fedha jumla ya program 27 (kati ya hizo saba ni mpya) na miradi ya maendeleo 77 (kati yake 11 ni mipya) yenye ghahama ya jumla ya shilingi bilioni 378.90, kati ya fedha hizo Serikali itatoa shilingi bilioni 37.95 sawa na asilimia 10 na washirika wa maendeleo watachangia shilingi bilioni 340.96 na kati ya hizo washirika wa maendeleo ruzuku ni shilingi bilioni 124.96 na mikopo shilingi bilioni 216.
Alieleza kwa upande wa matumizi kwa kila klasta ni pamoja na ukuzaji wa uchumi na upunguzaji wa umasikini inatarajiwa kutekeleza jumla ya program 17 (kati yake tano ni mpya) na miradi 17 (mmoja ni mpya) katika mwaka 2011/2012 kwa ghaama ya shilingi bilioni 183.23 kati ya hizo Serikali itatoa shilingi bilioni 15.76 na washirika wa maendeleo watachangia shilingi bilioni 167.48.
Waziri Omar alidokeza kwamba, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Serikali haikusudii kupandisha kodi yoyote, ambapo imekusudia kuimarisha zaidi usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa vianzio vilivyopo na kuziba mianya inayotumika katika kuepuka, kupunguza au kukwepa kulipa kodi pamoja na kuendelea kufuatilia matumizi mabaya ya misamaha ya kodi nchini.
Alisema lengo ni kuona kuwa kabla ya kuongeza kodi, juhudi zinachukuliwa katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji na uwajibikaji wa ulipaji kwenye vianzio vilivyopo na kuhakikisha kuwa misamaha inayotolewa inatumika kwa dhamira iliyokusudiwa.
“Katika juhudi za kuongeza na kuimarisha mapato ya Serikali katika mwaka ujao itaanza kupokea marejesho ya kodi ya mapato ya mtu binafsi kwa wafanyakazi wa taasisi za muungano wanaofanyakazi Zanzibar, ambapo hatua hii imekuja kufuatia makubaliano yaliofikiwa kati ya SMZ na SMT katika juhudi za kushughulikia kero za Muungano”, alisisitiza.
Alivitaja vipao mbele ni pamoja na kuimarisha huduma za afya kwa ununuzi wa vifaa vya hospitali na dawa, ubora wa elimu kwa kupunguza tatizo la uhaba wa madawati, vifaa vya maabara, maji safi na salama, kilimo cha umwagiliaji maji, mazingira bora ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na kuendeleza tafiti mbali mbali kwa lengo la kuimarisha uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii na maendeleo.
Alifahamisha kuwa, Serikali imepanga kuongeza mishahara kwa watumishi wake, hivyo mishahara na posho kwa Wizara na Idara za Serikali pamoja na taasisi zinazopokea ruzuku itakuwa ni shilingi bilioni 126.15 sawa na asilimia 53.9 ya matumizi yote ya kazi za kawaida ambayo ni asilimia 57.0 ya matarajio ya makusanyo ya mapato ya ndani.
Alisema kiwango hicho cha mishahara ni sawa na asilimia 11.5 ya pato la taifa ikilinganishwa na asilimia 9.9 kwa mwaka fedha ujao.
Waziri Omar alieleza kwa mwaka ujao wa fedha Serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni 613.08 ikilinganishwa na shilingi bilioni 444.64 kwa mwaka uliopita ikiwa ni ziada ya shilingi bilioni 168.44, hali hiyo inatokana na kuimarika kwa makusanyo ya ndani na kuongeza kwa misaada ya washirika wa maendeleo.

No comments:

Post a Comment