Monday 20 June 2011

AFYA ZA WANANCHI HATARINI.

Afya za wananchi hatarini

• Waendelea kuuziwa vyakula vibovu
Na Fatma Kassim, Maelezo Zanzibar
BODI ya Chakula Dawa na Vipodozi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamebaini kuwepo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu ambao hughushi tarehe ya matumizi katika vyakula vya makopo pamoja na vinywaji.
Wafanyabiashara hao wamebainika hivi karibuni kufuatia msako mkali na kufanikiwa kukamatwa mfanyabiashara mmoja katika maeneo ya Darajani Mjini Unguja na ambae anafanyiwa mahojiano na Jeshi la Polisi.
Mrajis wa Bodi hiyo Dk. Burhan Othman Simai, amesema wamefanikiwa kukamata makopo 456 ya Samli aina ya Chief Brand yenye ujazo wa kilo moja ambayo yalimaliza muda wa matumizi Februari mwaka huu na tarehe aliyoiweka ni 2012.
Bidhaa nyengine zilizokamatwa ni makopo kumi ya mananasi ya kopo pamoja na bidhaa mbali mbali za mchanganyiko ikiwemo sippy soda, maji na soda za aina ya potelo.
Bidhaa hizo baada kughushiwa tarehe huuzwa kwa bei rahisi katika Manispaa ya Zanzibar na sehemu mbali mbali na bila ya kuwa na utaalamu mtu hawezi kugundua tarehe hizo kwa urahisi.
Dk. Burhani amefahamisha kuwa mfanyabiashara huyo aliyekamatwa amekutwa na spray ambayo anatumia kwa kufutia tarehe na kuweka tarehe ya matumizi anayotaka yeye kwa kutumia makapen pamoja mihuri vijiti vya meno ambavyo hutumia kwa kuandikia.
Aidha alisema kuwa kwa kipindi kirefu Bodi yake imekuwa ikidhibiti bidhaa za Chakula vipodozi na madawa ambapo wameweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini bado wataendelea kufanya jitihada ya kuwakamata wale wote ambao wanahatarisha afya za wananachi.
Amewataka wananchi wote wa Unguja na Pemba kuwafichua wale wote wenye kufanya udanganyifu katika vyakukula, dawa na Vipodozi kwa lengo la kuwepo bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.
Bodi itaendelea kufanya misako mbali mbali ya madawa Vipodozi na kuhakikisha bidhaa zina ubora wa hali ya juu kwa watumiaji na kusitokee madhara yoyote.
Mbali ya ugunduzi huo, ripoti za uchunguzi zinaeleza kuwa bado kumezagaa biashara zilizopitwa na muda katika maduka mbali mbali Zanzibar, pamoja na dawa zilizopitwa na muda.

No comments:

Post a Comment