Monday, 20 June 2011

SERIKALI KUZIPA MSUKUMO JUMUIYA BINAFSI.

Serikali kuzipa msukumo jumuiya binafsi

Dk. Shein asema zitachapuza kasi ya maendeleo
Asisitiza umuhimu wa tafiti kuondosha umasikini
Na Mwantanga Ame
RAIS wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali itahakikisha inaziwekea mazingira mazuri na kuzisimamia jumuiya zinazoanzishwa kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya wananchi na nchi.
Dk. Shein alieleza hayo jana wakati akizindua Taasisi ya Sera za Umma (ZIRPP), katika ukumbi wa Salama uliopo hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Alisema serikali itazisiamia jumuia hizo ili ziweze kutekeleza dhamira, sera na mipango waliojiwekea katika kuwasaidia wananchi ili waweze kuondokana na umasikini.
Alifahamisha kuwa msaada wa serikali unahitajika kwani zipo jumuia zilizoshindwa kuutekeleza majukumu na kushindwa kuleta manufaa, ambapo alisema chanzo cha kutofanya vizuri ni ukosefu wa sera nzuri na kukosa malengo jambo ambalo serikali tayari inalifanyia kazi kwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala hilo.
Dk. Shein alisema Zanzibar ina jumuia za kiraia zilizosajiliwa rasmi 870 ambazo zimekuwa zikijihusisha na mambo mbali mbali katika jamii yakiwemo kibiashara, afya, elimu na ustawi wa jamii.
Kwa mara nyengine tena Dk.Shein alieleza umuhimu wa utafiti na kueleza kuwa tafiti zikifanyika vizuri zitaweza kubadili maisha ya Wazanzibari kwani hivi sasa tayari baadhi ya tafiti zilizofanywa katika sekta ya kilimo zimeonesha matokeo mazuri katika zao la mpunga baada ya kupatikana mbegu mpya ya NERICA.
Alisema mbegu hiyo inatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa katika kilimo cha zao hilo Wazanzibari watarajie makubwa katika bajeti ya wizara ya Kilimo ijayo kwani imedhamiria kukibadilisha kilimo na kukiweka katika taswira ya kisasa.
Dk. Shein alisema ili Zanzibar iendelee lazima igeukie eneo la utafiti na tafiti hizo zifanyiwe kazi ili ziweze kuleta manufaa kwa wananchi katika kuondokana na matatizo yanayowakabili.
Alifahamisha kuwa kwa kufahamu umuhimu wa utafiti serikali itashirikiana na serikali ya Muungano kwa kuendeleza utafiti na watafiti kwani tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya kuwapatia watafiti.
Alitoa wito kwa wataalamu kuchangamkia fedha hizo kutokana na hivi sasa kuonekana kuwepo kwa idadi ndogo ya Wazanzibari wanaojitokeza kuomba kwa ajili ya kufanyia utafiti huku kukiwa na maeneo kadhaa ambayo yanaweza kufanyiwa utafiti.
Dk. Shein alisema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, tayari kwa kushirikiana na wizara ya Sayansi na Teknologia na Mawasiliano ya Jamhuri ya Muungano Tanzania zimefanya mazungumzo ya pamoja kuhusu majukumu ya Tume ya Sayansi na Tekonologia katika kuendeleza masuala ya utafiti na kuwaendeleza watafiti.
Alisema serikali imo katika hatua ya kufungua ofisi itayoiwezesha COSTEC kufanya kazi zake hapa Zanzibar ambapo inatarajiwa kutoa elimu kuhusu mambo ya sera na sheria kwa watendaji wakuu wa serikali zitazokuwa zikiangalia mambo ya tafiti za Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Alisema sambamba na hilo ipo haja ya hivi sasa serikali kuanza kufanyiwa mapitio kamati zote za COSTEC ili kuingiza wataalamu wa Zanzibar.
Hatua hiyo Dk. Shein alisema pia itahitaji kuangaliwa kuundwa kwa chombo kimoja kwa kuanzisha Baraza la Utafiti Zanzibar ambacho kitakuwa ni msimamizi wa Mabaraza ya utafiti kutokana na yaliopo kuwa mbali mbali na yamekuwa yakifanya kazi kisekta.
Kutokana na na hatua hiyo Dk. Shein, aliiomba Jumuiya ya ZIRPP kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuhakikisha tafiti watazozifanya zinakuwa na wanufaa kwa wananchi wa Zanzibar na nchi yenywe.
Aidha aliomba Taasisi hiyo kuliangalia suala la kuwavuta wataalamu wa kizanzibari waliopo njia ya nchi kuona nao wanatoa mchango wao wa kitaaluma kwa serikali yao ili wachangie maendeleo ya nchi yao.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuia hiyo Maryam Hamdan, aliipongeza serikali kwa kushirikiana na taasisi hiyo kwa kukubali kuwa nayo pamoja.
Naye mlezi wa Jumuiya hiyo waziri Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Tanzania Dk. Salim Ahmed Salim, alisema taasisi hiyo itafanya utafiti wa kina juu ya mambo yanayowahusu vijana kutokana na hivi sasa ndio wanaokabiliwa na changamoto mbali mbali.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mohammed Yussuf, alisema taasisi hiyo ipo kwa ajili ya kubadili maendeleo ya Zanzibar na wananchi wake na haina mitazamo ya kisiasa kwani itahakikisha inapofanya kazi zake inashirikiana na serikali.
Alisema Jumuiya hiyo itahakikisha inawaunganisha wazanzibari popote walipo duniani ili waweze kuchangia uchumi wa nchi yao na kupunguza umasikini.
Uzinduzi wa Jumuiya hiyo ulihudhuriwa na wananchi mbali mbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Baraza la wawakilishi Pandu Ameir Kificho, Mkuu wa mkoa wa Mjini Abdalla Mwinyi Khamis, Mawaziri wa serikali ya Zanzibar, Makatibu Wakuu, vyama vya siasa, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Mjini Zanzibar na watafiti kutoka katika taasisi za utafiti Tanzania bara.

No comments:

Post a Comment