Tuesday 14 June 2011

MJADALA TVZ, HAJI AMEIR WANGUSA BAUSI

Mjadala TVZ, Haji Ameir wamgusa Baussi

Na Aboud Mahmoud
MWENYEKITI wa timu ya soka ya Wazee Sports Salum Baussi Nassor, ameeleza kukerwa na kitendo cha Makamu wa Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Haji Ameir, kuwaponda wanaokikosoa chama hicho kwa kuwataja kwa majina katika Televisheni Zanzibar.
Akizungumza na gazeti hili kufuatia kipindi cha Sunday Sports kilichorushwa na kituo cha TVZ hivi karibuni, alisema Ameir hakupaswa kuwakashifu wadau wa soka kwa kutumia chombo cha umma huku naye akiwa hana elimu ya kutosha wala ya utawala.
Alifahamisha kuwa kila nchi duniani inao watu wanaotumia wakati wao kufuatilia mambo mbalimbali, kuyatolea tathmini ikiwa pamoja na kukosoa na kupendekeza namna bora za kuleta ufanisi hasa endapo mambo hayo yanagusa maslahi ya umma.
Hata hivyo, alieleza kushangazwa, kwamba ZFA haiko tayari kukosolewa wala kusikiliza maoni na ushauri wa wadau wa soka ambao hufanya hivyo kwa kuona kuwa mchezo wa mpira wa miguu unaelekea kubaya, kwa kile alichodai mamlaka hiyo kuongozwa na watu wasiojali maendeleo yake.
“Kitendo cha Makamu huyo kuwapaka matope watu wanaoisaidia ZFA kwa kuizindua tena kupitia kioo cha televisheni ya taifa, si cha kiungwana, na hakikuzingatia nidhamu ya utawala, na kimeonesha ni namna gani kiongozi huyo hana dira”, alifafanua Bausi.
Bausi alisema wanachokifanya wadau wa soka ni kudhihirisha jinsi gani chama chenye dhamana ya kuendeleza mpira wa miguu kimejaa mapungufu na kufanya madudu ya makusudi lakini bado hakitaki kubadilika.
Akitoa mfano, alisema Ameir anawaambia Wazanzibari kuwa nchi yao itapata uanachama wa Shirikisho la Soka la Dunia ‘FIFA’, hali ya kuwa Rais wake Sepp Blatter hawezi kuzungumzia suala zito kama hilo pekee, bali kamati ndiyo inayojadili.
“Wasione hatufahamu, sisi tunafuatilia kila siku, nashangaa anawaongopea wananchi”, alieleza.
Aidha alikosoa kauli ya Makamu huyo kwamba FIFA inahitaji watu weledi wa soka na wanaoweza kuongoza, huku akijitolea mfano yeye Ameir kuwa ni miongoni mwa watu hao, akisema kauli hiyo inaonesha ubinafsi na kujikweza kwa sifa asizokuwa nazo.
Alifahamisha kuwa mambo kama hayo ya kuwakejeli wanaoikosoa ZFA, ndiyo yanayowakosanisha viongozi wa chama hicho na waandishi wa habari, ambao hivi karibuni kwa umoja wao waligomea kuhudhuria mkutano ulioitishwa na chama hicho wakitaka waombwe radhi.
Miongoni mwa watu waliotajwa na Ameir kupitia kipindi hicho, ni Salum Baussi, Maulid Hamad na Farouk Karim, na pale muendeshaji kipindi Abdallah Mussa alipomtaka asitaje watu kwa majina alitaka aachiwe na kutishia kuondoka.

No comments:

Post a Comment