Zanzibar kujenga bandari ya kisasa
Na Abdi Shamnah
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema serikali itajenga bandari mpya, ili kuondokana na changamoto kadhaa zinazoikabili bandari ya Malindi.
Alisema bandari itakayojengwa itakuwa kubwa na ya kisasa itakayoweza kutoa huduma kwa ufanisi, kulingana na teknolojia ya dunia ilivyo.
Maalim Seif alisema hayo jana Bandarini Malindi mjini hapa alipokuwa na mazungumzo na Bodi ya Wakurugenzi pamoja na watendaji wakuu wa Shirika hilo, kufuatia ziara yake ya kuangalia shughuli zinazoendeshwa na Shirika pamoja na changamoto mbali mbali zinazokabili.
Alifahamisha kuwa suluhisho pekee la kuondokana na changamoto kadhaa zinazoikabili Bandari hiyo, ikiwemo ufinyu wa nafasi na miundombinu chakavu ni kupata Bandari mpya itayojengwa kulingana na mahitaji ya nchi na kwa wakati uliiopo.
Alisema serikali inaendelea na mazungumzo na washirika wa maendeleo kusaidia mpango huo ili kuimarisha biashara na kukuza uchumi wa Taifa.
Alitaka menejimenti ya Shirika hilo kuendelea na juhudi za kuliimarisha Shirika na kukabiliana na changamoto zilizo ndani ya uwezo wao ikiwemo kuongeza mapato, kujiendesha kibiashara na kuleta ushindani kwa Bandari nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki za Mombasa, Tanga na Dar es Salaam.
Akigusia uimarishaji wa Bandari ndogo ndogo zilizo chini ya Shirika hilo, hususan ile ya Mkokotoni, Maalim Seif alishauri utafiti wa kutosha ufanyike ili kuangalia faida itakayopatikana katika ujenzi wa Bandari hiyo, baada ya kuibuka kwa mawazo mapya ya kujengwa katika eneo la Fukuchani badala ya Mkokotoni.
Katika hatua nyingine Maalim Seif alisisitiza umuhimu wa menejimenti hiyo kuzingatia suala la usalama wa Bandari kwa kuweka udhibiti wa kutosha kukabiliana na uingiaji holela wa watu banadarini.
Alisema katika utekelezaji wa jambo hilo, elimu ya kutosha inapaswa kutolewa ili wananchi waelewe umuhimu na ‘unyeti’ wa eneo hilo na kuondokana na dhana ya kuwa wanasumbuliwa pale wanapofanyiwa ukaguzi wa mizigo yao.
Mapema waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Hamad Masoud alisema Bandari hiyo ilikuwa katika hatari ya kukimbiwa na meli kutoka nje kwa kukosa usalama wa kutosha, kulingana na masharti ya I.M.O.
Hata hivyo alisema juhudi kubwa zimechukuliwa kuzipatia ufumbuzi baadhi ya kasoro zilizokuwepo, na kuainisha kuibuka kwa manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wananchi, wakihisi kusumbuliwa kufuatia utaratibu wa kuwekwa vitambulisho.
Naye Mkurugenzi wa Shirika hilo, Mustapha Aboud Jumbe, alimweleza Makamu wa Rais juu ya changamoto kadhaa zinazolikabili shirika hilo, ikiwemo ufinyu wa eneo la bandari na uchakavu wa miundo mbinu, mlundikano wa makontena matupu, ongezeko la uzito wa meli, usalama wa meli hususan zile za kitalii, ukosefu wa taa katika minara na maboya.
Alisema malengo ya Shirika kuwa na mradi wa kutumia nishati ya jua (solar power) katika minara yake Unguja na Pemba, badala ya gesi na kuweka kando matumizi ya umeme ambao una gharama kubwa.
Katika ziara hiyo, Maalim Seif alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali, ikiwemo eneo la Abiria na tishali la vyombo, sehemu ya kuhudumia vyombo vya ufukweni (landing Craft), kuangalia ukuta wa Forodhani ulioathirika na mawimbi ya Bahari, eneo la majahazi, karakana ya Shirika, eneo la kupitishia mashine za usalama (screen area) pamoja na eneo la Bwawani lililofukiwa na kutumika kwa ajili ya kuhifadhia Makontena.
Monday, 13 June 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment