Friday, 17 June 2011

ZFA PEMBA, ZANZIBAR OCEAN VIEW USANII MTUPU.

 ZFA Pemba, Zanzibar Ocean View usanii mtupu

Ni kutokana na faini iliyotozwa Zanzibar Ocean View
Na Salum Vuai, Maelezo
LICHA ya uongozi wa klabu ya Zanzibar Ocean View kudai umeshalipa faini iliyotozwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Pemba, uongozi wa chama hicho umesema haujapokea fedha hizo na kuamua kuiongezea adhabu.
Awali, Zanzibar Ocean View ilitakiwa ilipe faini ya shilingi 620,000 katika ofisi za ZFA Pemba na si kwengineko, ikiwa adhabu ya kutokwenda kucheza mechi yake ya mwisho ya ligi ndogo dhidi ya Duma Juni 6, mwaka huu, si zaidi ya Juni 14.
Alipoulizwa iwapo klabu yake imeshalipa ili kuepuka faini mara mbili pamoja na kuteremshwa daraja, Katibu Mkuu wa timu hiyo Hashim Salum, alidai klabu yake imeuagiza uongozi wa ZFA Taifa Unguja, kukata fedha hizo katika deni inalodaiwa na Zanzibar Ocean View.
Hata hivyo, Hashim hakuonesha vielelezo vya barua inayokitaka chama hicho kuchukua hatua hiyo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Pemba, Msaidizi Katibu Mkuu wa ZFA Taifa Pemba Kassim Haji Salum, amesema kamati yake ilikutana juzi kujadili kitendo cha klabu hiyo kushindwa kulipa faini na kuamua kuiongezea adhabu mara mbili zaidi.
Salum alieleza kuwa kutokana na tabia hiyo kujirudia kwa klabu hiyo, chama hicho kimeamua kuipiga faini ya shilingi 3,440,000 kwa mujibu wa kanuni ya ZFA namba 20 a (i), ambayo imetakiwa kulipa si zaidi ya Juni 22, mwaka huu katika ofisi za ZFA Gombani Pemba.
Alifahamisha kuwa endapo tena Zanzibar Ocean View haitalipa faini hiyo, itateremshwa daraja hadi la kwanza taifa pamoja na kutakiwa ilipe kama inavyoelekeza kanuni ya chama hicho namba 20 a (iii).
Kwa mara nyengine, Msaidizi Katibu huyo alisisitiza kwamba faini hiyo ni lazima ilipwe Pemba kwani asilimia 50 ya fedha hizo, zinahitajiwa kwenda kwa klabu husika ambayo ilikuwa icheze na timu hiyo iliyoshindwa kufika uwanjani.
Kassim alisema tayari chama chake kimeuandikia barua uongozi wa Zanzibar Ocean View na kwamba anaamini hautapuuza kutimiza agizo hilo.
Tangu Zanzibar Ocean View iliposhindwa kwenda Pemba kumaliza mechi za ligi ndogo dhidi ya Duma, pande mbili hizo zimekuwa zikioneshana umwamba unaoonekana kama mchezo wa kuigiza.

No comments:

Post a Comment