Monday 20 June 2011

ZFA KUTIMULIWA BWAWANI

ZFA kutimuliwa Bwawani

Ni kwa kushindwa kulipa kodi 2.4m/-
Na Mwantanga Ame
KUFUATIA kushindwa kulipa kodi kwa muda mrefu sasa, Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), huenda kikatimuliwa katika ofisi ilizokodishwa ndani ya majengo ya hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Chama hicho kimekuwa kikifanya shughuli zake hotelini humo tangu kilipoondoshwa katika ofisi za uwanja wa Amaan, ambao ulikuwa ukifanyiwa matengenezo.
Taarifa za ndani zilizopatikana kutoka kwa uongozi wa hoteli hiyo, zimefahamisha kuwa kadhia ya deni la ZFA imefikishwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, kwa hatua zaidi baada kumalizika muda wa awali uliopewa chama hicho kulipa deni inalodaiwa.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa, hapo awali uongozi wa hoteli hiyo ulizipa notisi taasisi zote zilizopangishwa hotelini humo ambazo zina madeni, na kuzitaka kuyasawazisha hadi ifikapo Juni 1, mwaka huu, na kwamba baadhi yao zimeanza kutekeleza agizo hilo.
Mkurugenzi Mipango wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Joseph Kilangi, amekiri kuwepo wadaiwa sugu katika hoteli hiyo, ikiwemo ZFA ambayo licha ya kukumbushwa kwa barua, haijalipa wala kutoa kauli yoyote.
Kilangi alisema kuwa deni la chama hicho kinachoongoza mchezo wa mpira wa miguu nchini, limefikia shilingi milioni 2.4.
Hata hivyo, Kilangi alisema wizara yake inakusudia kuwakumbusha tena wadaiwa wote ikiwemo ZFA juu ya umuhimu wa kulipa madeni yao, na atakaeshindwa hadi kufikia mwezi Julai, atatimuliwa pamoja na kufilisiwa mali zake.
"Tunakusudia kuendesha zoezi la kuwaondoa wapangaji hao kistaarabu kwa kuzingatia sheria ili tusije kukiuka mikataba ya wakodishwaji hao na kuiingiza serikali katika matatizo kama ilivyotokea kwa Pemba Bar", alisema Kilangi.
“Tutawaandikia barua walipe deni lao kama wameshindwa basi watatuwia radhi, itawabidi watoke ili tuingie mikataba na watu wengine”, alisema Mkurugenzi huyo.
Uamuzi wa wizara unafuatia ziara ya hivi karibuni ya Kamati ya Mifugo, Uwezeshaji, Utalii na Habari ya Baraza la Wawakilishi iliyokuwa ikiongozwa Asha Bakari Makame, ambapo iliitaka wizara hiyo kuchukua hatua ya kuwaondoa wadaiwa sugu wa hoteli hiyo.

No comments:

Post a Comment