Monday, 20 June 2011

CONGO YAIDUWAZA UHOLANZI FIFA U-17

Congo yaiduwaza Uholanzi FIFA U-17

MEXICO CITY
CONGO imeanza kwa kishindo fainali za Kombe la Dunia kwa vijana walio chini ya miaka 17 kwa kuwafunga mabingwa watetezi Uholanzi kwa bao 1-0 mjini Morelia.
Ingawa Uholanzi ilitawala katika kipindi cha kwanza, Congo iliweza kujipatia bao lake lililofungwa na Justalain Kounkou mnamo dakika ya 53.
Matokeo hayo yanaifanya Congo kushika nafasi ya pili katika kundi A, nyuma ya wenyeji Mexico walioifunga Korea ya Kaskazini magoli 3-1 katika mchezo wa ufunguzi.
Huo ni ushindi wa kwanza kwa Congo katika ngazi hiyo tangu mwaka 1991 walipoichapa Mexico, ambayo watakabiliana nayo kesho.
Hata hivyo, katika mchezo huo, nyavu za ‘The Baby Red Devils’, Congo, zilitikishwa katikati ya kipindi cha kwanza na mchezaji Tonny Trindade de Vilhena, lakini bao hilo lilikataliwa na muamuzi kwa madai kuwa mfungaji alikuwa ameotea.
Baada ya Wakongo ambao walimaliza wa tatu katika fainali za mataifa ya Afrika mwezi Januari kujipatia bao, walikuwa wakicheza kwa utulivu na kuwanyanyasa wapinzani wao kama walivyotaka.

No comments:

Post a Comment